Mathayo 24:32-44
Mathayo 24:32-44 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina. Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja. Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu. Lakini kumbukeni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”
Mathayo 24:32-44 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mnatambua ya kuwa wakati wa mavuno uko karibu; nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yote, tambueni ya kuwa yuko karibu, katika malango. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia. Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Lakini kuhusu siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako shambani; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliujua ule wakati mwizi atakaokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyotazamia Mwana wa Adamu yuaja.
Mathayo 24:32-44 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia. Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
Mathayo 24:32-44 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yote, mtambue kwamba wakati u karibu, hata malangoni. Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. Kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile Nuhu alipoingia katika safina. Nao hawakujua lolote hadi gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu. Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wanasaga kwa kinu cha mkono, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.