Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 24

24
Kuharibiwa kwa hekalu kwatabiriwa
1 # Mk 13:1-37; Lk 21:5-36 Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya hekalu. 2#Lk 19:44 Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa.
Ishara za mwisho wa nyakati
3Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? 4Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. 5#Mt 24:24; Yn 5:43; Mdo 5:36,37; 1 Yoh 2:18 Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. 6#Dan 2:28 Nanyi mtasikia habari za vita na tetesi za vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. 7#Isa 19:2; 2 Nya 15:6 Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8Hayo yote ndiyo mwanzo wa uchungu.
Mateso yatabiriwa
9 # Mt 10:17,22; Yn 16:2 Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. 10#Dan 11:41 Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. 11#Mt 7:15; 1 Yoh 4:1 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. 12#2 The 2:10; 2 Tim 3:1-5 Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapunguka. 13#Mt 10:22; Ufu 13:10 Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. 14#Mt 28:19; 10:18 Tena Habari Njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
Chukizo la Uharibifu
15 # Dan 9:27; 11:31; 12:11 Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), 16ndipo walio katika Yudea na wakimbilie milimani; 17#Lk 17:31 naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; 18wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. 19Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! 20#Mdo 1:12 Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. 21#Dan 12:1; Ufu 7:14; Yoe 2:2 Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. 22Na kama siku hizo zisingalifupishwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupishwa. 23Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. 24#Mt 5:11; Kum 13:1-3; 2 The 2:8,9 Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwezekana, hata walio wateule. 25Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. 26#Lk 17:23-24 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. 27Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28#Ayu 39:30; Hab 1:8; Lk 17:37 Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Kuja kwa Mwana wa Adamu
29 # Isa 13:10; 34:4; Eze 32:7; Yoe 2:10; 3:4; 3:15; Ufu 6:12-13; 2 Pet 3:10 Lakini mara tu, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka kutoka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; 30#Dan 7:13; Zek 12:10-14; Ufu 1:7; 19:11; Mt 26:64 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. 31#1 Kor 15:52; 1 The 4:16; Ufu 8:1,2; Isa 27:13; Zek 2:6; Kum 30:4 Naye atawatuma malaika wake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.
Funzo kutoka kwa mtini
32Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mnatambua ya kuwa wakati wa mavuno uko karibu; 33nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yote, tambueni ya kuwa yuko karibu, katika malango. 34Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia. 35#Mt 5:18 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Haja ya kuwa waangalifu
36 # 1 The 5:1,2 Lakini kuhusu siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. 37#Mwa 6:5-8; Lk 17:26,27 Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38#2 Pet 3:5,6; Mwa 7:7 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, 39#Mwa 7:6-24 wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 40#Lk 17:35,36 Wakati ule watu wawili watakuwako shambani; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; 41wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 # Mt 25:13 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. 43#Lk 12:39-40 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliujua ule wakati mwizi atakaokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. 44#Ufu 16:15 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyotazamia Mwana wa Adamu yuaja.
Mtumwa mwaminifu au asiye mwaminifu
45Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? 46Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. 47#Mt 25:21,23 Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. 48#Mhu 8:11 Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; 49akaanza kuwapiga watumwa wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi; 50bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyotazamia, na saa asiyojua, 51#Mt 8:12 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Iliyochaguliwa sasa

Mathayo 24: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha