Mathayo 24:22-34
Mathayo 24:22-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa. “Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: ‘Kristo yuko hapa’ au ‘Yuko pale,’ msimsadiki. Maana watatokea akina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. Sikilizeni, nimekwisha waonya kabla ya wakati. Basi, wakiwaambieni, ‘Tazameni, yuko jangwani,’ msiende huko; au, ‘Tazameni, amejificha ndani,’ msisadiki; maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. “Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu. “Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.
Mathayo 24:22-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na kama siku hizo zisingalifupishwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwezekana, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. Lakini mara tu, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka kutoka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika wake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu. Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mnatambua ya kuwa wakati wa mavuno uko karibu; nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yote, tambueni ya kuwa yuko karibu, katika malango. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.
Mathayo 24:22-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu. Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.
Mathayo 24:22-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna mtu ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. Tazameni, nimekwisha kuwaambia mapema. “Basi mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. Kwa maana kama vile radi itokavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai. “Mara baada ya dhiki ya siku zile, “ ‘jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’ “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu. Naye atawatuma malaika wake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine. “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yote, mtambue kwamba wakati u karibu, hata malangoni. Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.