Mathayo 24:1-28
Mathayo 24:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alitoka hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonesha majengo ya hekalu. Yesu akawaambia, “Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.” Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?” Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watatokea wakisema kila mmoja kwamba yeye ndiye Kristo nao watawapotosha watu wengi. Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi. Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto. “Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa sababu ya jina langu. Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi. Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote. “Basi, mtakapoona ‘Chukizo Haribifu lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato! Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena. Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa. “Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: ‘Kristo yuko hapa’ au ‘Yuko pale,’ msimsadiki. Maana watatokea akina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. Sikilizeni, nimekwisha waonya kabla ya wakati. Basi, wakiwaambieni, ‘Tazameni, yuko jangwani,’ msiende huko; au, ‘Tazameni, amejificha ndani,’ msisadiki; maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Mathayo 24:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa. Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na tetesi za vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa uchungu. Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapunguka. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena Habari Njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Yudea na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupishwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwezekana, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Mathayo 24:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu. Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Mathayo 24:1-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya Hekalu. Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.” Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?” Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi. Mtasikia habari za vita na tetesi za vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa uchungu. “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu, upendo wa watu wengi utapoa, lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. Injili hii ya ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja. “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), basi wale walio Yudea wakimbilie milimani. Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwepo tangu mwanzo wa dunia hadi sasa: wala haitakuwepo tena kamwe. “Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna mtu ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. Tazameni, nimekwisha kuwaambia mapema. “Basi mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. Kwa maana kama vile radi itokavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.