Mathayo 22:27-40
Mathayo 22:27-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake. Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu, “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?” Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’. Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza. Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’. Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili.”
Mathayo 22:27-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi kati ya wale saba? Maana wote walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Mnapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kuhusu kiyama ya wafu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake. Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea Torati yote na vitabu vya Manabii.
Mathayo 22:27-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake. Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.
Mathayo 22:27-40 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?” Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Wale umati wa watu waliposikia hayo, walishangaa sana kwa mafundisho yake. Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja. Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?” Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”