Mathayo 22:23-33
Mathayo 22:23-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu. Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.
Mathayo 22:23-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi kati ya wale saba? Maana wote walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Mnapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kuhusu kiyama ya wafu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake.
Mathayo 22:23-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake.
Mathayo 22:23-33 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema, “Mwalimu, Musa alisema, ‘Mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’ Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane. Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba. Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?” Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Wale umati wa watu waliposikia hayo, walishangaa sana kwa mafundisho yake.