Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 22:1-46

Mathayo 22:1-46 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano: “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi. Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’ Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua. Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumishi wake: ‘Karamu ya harusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili. Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje harusini.’ Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya harusi ikajaa wageni. “Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya harusi. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya. Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.” Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?” Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu? Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha. Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao. Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu. Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake. Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu, “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?” Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’. Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza. Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’. Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili.” Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza, “Nyinyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Wa Daudi.” Yesu akawaambia, “Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.’ Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo ‘Bwana,’ anawezaje kuwa mwanawe?” Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.

Shirikisha
Soma Mathayo 22

Mathayo 22:1-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mifano, akisema, Ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawadhulumu na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akatuma majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi iko tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi Nendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache. Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, tunajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao. Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi kati ya wale saba? Maana wote walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Mnapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kuhusu kiyama ya wafu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake. Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea Torati yote na vitabu vya Manabii. Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mnaonaje kuhusu Kristo? Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi. Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi katika mkono wangu wa kulia, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako? Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe? Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu yeyote tangu siku ile kumwuliza neno tena.

Shirikisha
Soma Mathayo 22

Mathayo 22:1-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache. Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao. Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake. Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii. Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo? Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi. Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako? Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe? Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena.

Shirikisha
Soma Mathayo 22

Mathayo 22:1-46 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja. “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’ “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto. “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni. “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema. “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’ “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.” Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake. Wakatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode kwake. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonesha upendeleo. Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” Lakini Yesu alifahamu kusudi lao mbaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? Nionesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao. Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema, “Mwalimu, Musa alisema, ‘Mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’ Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane. Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba. Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?” Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Wale umati wa watu waliposikia hayo, walishangaa sana kwa mafundisho yake. Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja. Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?” Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.” Mafarisayo wakiwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza, “Mnaonaje kuhusu Kristo? Yeye ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.” Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema, “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.”’ Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.

Shirikisha
Soma Mathayo 22