Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 21:1-22

Mathayo 21:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu. Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji,’ naye atawaachieni mara.” Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie: “Uambieni mji wa Siyoni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda.” Hivyo, wale wanafunzi walikwenda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza. Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake. Umati mkubwa wa watu wakatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani. Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti: “Sifa kwa Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Sifa kwa Mungu juu!” Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, “Huyu ni nani?” Watu katika ule umati wakasema, “Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti mji wa Galilaya.” Basi, Yesu akaingia hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi.” Vipofu na vilema wengine walimwendea huko hekaluni, naye Yesu akawaponya. Basi, makuhani wakuu na waalimu wa sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaza sauti zao hekaluni wakisema: “Sifa kwa Mwana wa Daudi,” wakakasirika. Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjapata kusoma Maandiko haya? ‘Kwa vinywa vya watoto wadogo na wachanga wajipatia sifa kamili.’” Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko. Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauna chochote ila majani matupu. Basi, akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka. Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ itafanyika hivyo. Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba kwa sala, mtapata.”

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Nendeni katika kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; naye atawatuma mara moja. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwanapunda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwanapunda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya. Yesu akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa; akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Na vipofu na viwete wakamwendea mle hekaluni, akawaponya. Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika, wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umejiandalia sifa? Akawaacha, akatoka nje ya mji mpaka Bethania, akalala huko. Na asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara. Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara? Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yoyote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya. Yesu akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa; akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Na vipofu na viwete wakamwendea mle hekaluni, akawaponya. Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika, wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa? Akawaacha, akatoka nje ya mji mpaka Bethania, akalala huko. Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara. Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara? Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu, nanyi mtampata punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. Mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara moja.” Haya yalitukia ili litimie neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mpole, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’” Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza. Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake. Umati mkubwa wa watu wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kwenye miti, wakayatandaza barabarani. Wale umati wa watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti na kusema, “Hosana, Mwana wa Daudi!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Hosana juu mbinguni!” Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?” Wale umati wa watu wakajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti ya Galilaya.” Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.” Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya, na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu, wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika. Wakamuuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya umeamuru sifa’?” Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko. Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka. Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?” Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”

Shirikisha
Soma Mathayo 21