Mathayo 21:1-22
Mathayo 21:1-22 NENO
Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu, nanyi mtampata punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. Mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara moja.” Haya yalitukia ili litimie neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mpole, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’” Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza. Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake. Umati mkubwa wa watu wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kwenye miti, wakayatandaza barabarani. Wale umati wa watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti na kusema, “Hosana, Mwana wa Daudi!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Hosana juu mbinguni!” Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?” Wale umati wa watu wakajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti ya Galilaya.” Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.” Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya, na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu, wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika. Wakamuuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya umeamuru sifa’?” Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko. Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka. Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?” Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”