Mathayo 2:19-23
Mathayo 2:19-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.” Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli. Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya, akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.”
Mathayo 2:19-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Herode alipofariki, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Inuka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akainuka akamchukua mtoto na mamaye, akaenda katika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anatawala huko Yudea mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazareti.
Mathayo 2:19-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.
Mathayo 2:19-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yusufu katika ndoto huko Misri na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wakijaribu kumuua mtoto wamekufa.” Basi Yusufu, akainuka, akamchukua mtoto na mama yake wakaenda hadi nchi ya Israeli. Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Yudea baada ya Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Kwa kuwa alikuwa ameonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya, akaenda kuishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii waliposema, “Ataitwa Mnazareti.”