Mathayo 2:16-23
Mathayo 2:16-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia: “Sauti imesikika huko Rama, kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote wamefariki.” Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.” Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli. Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya, akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.”
Mathayo 2:16-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale majusi, alighadhibika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wa kiume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake kote, kuanzia wenye miaka miwili na chini yake, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale majusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawapo tena. Herode alipofariki, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Inuka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akainuka akamchukua mtoto na mamaye, akaenda katika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anatawala huko Yudea mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazareti.
Mathayo 2:16-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako. Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.
Mathayo 2:16-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Herode alipogundua kwamba alikuwa amedanganywa na wale wataalamu wa nyota, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kwa mujibu wa ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, aliposema: “Sauti ilisikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akilia kwa ajili ya wanawe, akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.” Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yusufu katika ndoto huko Misri na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wakijaribu kumuua mtoto wamekufa.” Basi Yusufu, akainuka, akamchukua mtoto na mama yake wakaenda hadi nchi ya Israeli. Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Yudea baada ya Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Kwa kuwa alikuwa ameonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya, akaenda kuishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii waliposema, “Ataitwa Mnazareti.”