Mathayo 2:13-21
Mathayo 2:13-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokuambia, maana Herode anakusudia kumuua huyu mtoto.” Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri. Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie: “Nilimwita Mwanangu kutoka Misri.” Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia: “Sauti imesikika huko Rama, kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote wamefariki.” Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.” Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli.
Mathayo 2:13-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hadi nitakapokuambia; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hadi Herode alipokufa; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nilimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale majusi, alighadhibika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wa kiume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake kote, kuanzia wenye miaka miwili na chini yake, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale majusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawapo tena. Herode alipofariki, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Inuka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akainuka akamchukua mtoto na mamaye, akaenda katika nchi ya Israeli.
Mathayo 2:13-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako. Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.
Mathayo 2:13-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yusufu katika ndoto akamwambia, “Amka, umchukue mtoto na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko hadi nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.” Kisha Yusufu akaamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri, ambako walikaa hadi Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile neno Bwana alilosema kupitia kwa nabii: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.” Herode alipogundua kwamba alikuwa amedanganywa na wale wataalamu wa nyota, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kwa mujibu wa ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, aliposema: “Sauti ilisikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akilia kwa ajili ya wanawe, akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.” Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yusufu katika ndoto huko Misri na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wakijaribu kumuua mtoto wamekufa.” Basi Yusufu, akainuka, akamchukua mtoto na mama yake wakaenda hadi nchi ya Israeli.