Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 2:1-23

Mathayo 2:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, wakauliza, “Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. Basi, akawaita pamoja makuhani wakuu wote na waalimu wa sheria, akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?” Nao wakamjibu, “Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika: ‘Ee Bethlehemu nchini Yudea, wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu, Israeli.’” Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, “Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende kumwabudu.” Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: Dhahabu, ubani na manemane. Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine. Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokuambia, maana Herode anakusudia kumuua huyu mtoto.” Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri. Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie: “Nilimwita Mwanangu kutoka Misri.” Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia: “Sauti imesikika huko Rama, kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote wamefariki.” Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.” Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli. Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya, akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.”

Shirikisha
Soma Mathayo 2

Mathayo 2:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, majusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Yudea; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe miongoni mwa watawala wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale majusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. Akawatuma Bethlehemu, akasema, Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, mpaka iliposimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu, uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hadi nitakapokuambia; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hadi Herode alipokufa; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nilimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale majusi, alighadhibika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wa kiume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake kote, kuanzia wenye miaka miwili na chini yake, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale majusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawapo tena. Herode alipofariki, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Inuka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akainuka akamchukua mtoto na mamaye, akaenda katika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anatawala huko Yudea mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazareti.

Shirikisha
Soma Mathayo 2

Mathayo 2:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako. Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.

Shirikisha
Soma Mathayo 2

Mathayo 2:1-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Yudea, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni wapi ambapo Kristo angezaliwa. Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Yudea, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii: “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, wewe si mdogo miongoni mwa watawala wa Yuda; kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala atakayekuwa mchungaji wa watu wangu Israeli.’” Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. Kisha akawatuma Bethlehemu na kuwaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto huyo kwa makini. Mara tu mtakapompata, nileteeni taarifa ili nami niende kumwabudu.” Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata hadi iliposimama mahali alipokuwa mtoto. Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mama yake, wakamsujudia na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. Kwa kuwa walikuwa wameonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi nchi yao kwa njia nyingine. Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yusufu katika ndoto akamwambia, “Amka, umchukue mtoto na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko hadi nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.” Kisha Yusufu akaamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri, ambako walikaa hadi Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile neno Bwana alilosema kupitia kwa nabii: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.” Herode alipogundua kwamba alikuwa amedanganywa na wale wataalamu wa nyota, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kwa mujibu wa ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, aliposema: “Sauti ilisikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akilia kwa ajili ya wanawe, akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.” Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yusufu katika ndoto huko Misri na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wakijaribu kumuua mtoto wamekufa.” Basi Yusufu, akainuka, akamchukua mtoto na mama yake wakaenda hadi nchi ya Israeli. Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Yudea baada ya Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Kwa kuwa alikuwa ameonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya, akaenda kuishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii waliposema, “Ataitwa Mnazareti.”

Shirikisha
Soma Mathayo 2