Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 2:1-11

Mathayo 2:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Yudea, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni wapi ambapo Kristo angezaliwa. Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Yudea, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii: “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, wewe si mdogo miongoni mwa watawala wa Yuda; kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala atakayekuwa mchungaji wa watu wangu Israeli.’” Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. Kisha akawatuma Bethlehemu na kuwaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto huyo kwa makini. Mara tu mtakapompata, nileteeni taarifa ili nami niende kumwabudu.” Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata hadi iliposimama mahali alipokuwa mtoto. Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mama yake, wakamsujudia na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.

Shirikisha
Soma Mathayo 2