Mathayo 16:1-12
Mathayo 16:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni. Lakini Yesu akawajibu, [“Ikifika jioni nyinyi husema: ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!’ Na alfajiri mwasema: ‘Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda!’ Basi, nyinyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia hali ya anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.] Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ile ya Yona.” Basi, akawaacha, akaenda zake. Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate. Yesu akawaambia, “Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!” Lakini wao wakawa wanajadiliana: “Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate.” Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu 5,000? Je, mlijaza vikapu vingapi vya mabaki? Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu 4,000, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki. Mbona hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!” Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Mathayo 16:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara itokayo mbinguni. Akajibu, akawaambia, [Jioni ikifika, mnasema, hali ya anga itakuwa mzuri; kwa kuwa mbingu ni nyekundu. Na asubuhi, mnasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mnajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za nyakati hizi hamwezi kuzitambua?] Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake. Nao wanafunzi wakaenda hadi ng'ambo, wakasahau kuchukua mikate. Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate. Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani haba, kwa sababu hamna mikate? Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota? Wala ile mikate saba kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota? Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa sikuwaambia kwa sababu ya mkate? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Mathayo 16:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni. Akajibu, akawaambia, [Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu. Na asubuhi, mwasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?] Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake. Nao wanafunzi wakaenda hata ng’ambo, wakasahau kuchukua mikate. Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate. Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu hamna mikate? Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota? Wala ile mikate saba kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota? Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Mathayo 16:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni. Yesu akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’ Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua ishara za nyakati. Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake. Wanafunzi wake walipofika ngʼambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate. Yesu akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.” Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.” Yesu, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano kwa watu elfu tano, na idadi ya vikapu vilivyojaa mabaki mlivyokusanya? Au ile mikate saba kwa watu elfu nne na idadi ya vikapu vilivyojaa mabaki mlivyokusanya? Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi kuhusu chachu ya kutengeneza mikate, bali kuhusu mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.