Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 14:1-36

Mathayo 14:1-36 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu. Basi, akawaambia watumishi wake, “Mtu huyu ni Yohane Mbatizaji, amefufuka kutoka kwa wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Kisa ni kwamba Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!” Herode alitaka kumuua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii. Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, “Nipe papa hapa katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu. Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini. Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao. Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na saa za mchana zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Si lazima waende, wapeni nyinyi chakula.” Lakini wao wakamwambia, “Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili.” Yesu akawaambia, “Nileteeni hapa.” Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ngambo ya ziwa wakati yeye anayaaga makundi ya watu. Baada ya kuwaaga watu, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, na wakati huo ile mashua ilikwisha fika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikumbwa na taabu kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliogopa sana, wakasema, “Ni mzimu!” Wakapiga yowe kwa hofu. Mara, Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” Petro akamwambia, “Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako.” Yesu akasema, “Haya, njoo.” Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, “Bwana, niokoe!” Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, “Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?” Kisha wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.” Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti. Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote, wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona.

Shirikisha
Soma Mathayo 14

Mathayo 14:1-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi karamuni pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule msichana; akakileta kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari. Naye Yesu aliposikia hayo, aliondoka huko katika mashua, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto. Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande katika mashua na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na ile mashua imekwisha kufika katikati ya bahari, inapigwa sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa unawakabili. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni mzimu; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo, ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka katika mashua, akatembea juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda katika mashua, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya mashua wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu. Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti. Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa wagonjwa; nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.

Shirikisha
Soma Mathayo 14

Mathayo 14:1-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari. Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto. Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu. Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti. Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa hawawezi; nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.

Shirikisha
Soma Mathayo 14

Mathayo 14:1-36 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, kwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” Herode alitaka sana kumuua Yohana, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii. Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria. Alimfurahisha Herode sana, kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” Mfalme alisikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake, wakamzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu. Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makundi makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao. Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makundi ya watu ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.” Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.” Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” Yesu akaagiza umati wa watu wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia ule umati. Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto. Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua wamtangulie kwenda ngʼambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiaga ule umati. Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake. Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa. Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.” Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.” Yesu akamwambia, “Njoo.” Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, akapaza sauti na kusema, “Bwana, niokoe!” Mara Yesu akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?” Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Yesu, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti. Watu wa eneo lile walipomtambua Yesu, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakamletea wagonjwa wao wote, wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

Shirikisha
Soma Mathayo 14