Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:37-50

Mathayo 13:37-50 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu akawaambia, “Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu. Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu. Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika. Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati; Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu, na kuwatupa katika tanuri ya moto, na huko watalia na kusaga meno. Kisha, wale wema watangara kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie! “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri. Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: Malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema, na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.”

Shirikisha
Soma Mathayo 13

Mathayo 13:37-50 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie. “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua. “Tena, ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. Ulipojaa, wavuvi wakauvuta ufuoni, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

Shirikisha
Soma Mathayo 13