Mathayo 13:1-32
Mathayo 13:1-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa. Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashuani, akaketi. Watu wote walisimama kwenye ukingo wa ziwa, naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano. “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, ziliteketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga. Nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: Nyingine punje mia, nyingine sitini na nyingine thelathini. Mwenye masikio na asikie!” Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. Ndio maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi. Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya: ‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa. Kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.’ “Lakini heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia. Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie. “Basi, nyinyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi. Yeyote asikiaye neno juu ya ufalme wa Mungu bila kuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na mara akalipokea kwa furaha. Lakini halishiki na mizizi ndani yake; huendelea kulizingatia neno hilo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya neno hilo, anakata tamaa mara. Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali hulisonga neno hilo, naye hazai matunda. Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na kuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini.” Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake. Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana. Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, ‘Bwana, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?’ Yeye akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya hivyo’. Basi, watumishi wake wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayangoe?’ Naye akawajibu, ‘La, msije labda mnapokusanya magugu, mkangoa na ngano pia. Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.’” Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake. Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikisha ota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.”
Mathayo 13:1-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda katika mashua, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Na alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; zikaota haraka, kwa kukosa udongo wenye kina; Lakini jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio na asikie. Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini yeyote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie. Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. Kila mtu alisikiapo neno la ufalme bila kulielewa, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kulielewa; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika shamba lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hadi wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko miboga yote ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kukaa katika matawi yake.
Mathayo 13:1-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio na asikie. Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie. Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.
Mathayo 13:1-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku hiyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari. Umati mkubwa mno wa watu wakakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari. Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini. Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.” Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Akawajibu, “Ninyi mmepewa ujuzi wa siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawajapewa. Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa. Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano: “Ingawa wanatazama, hawaoni; wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi. Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema: “ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama lakini hamtaona. Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’ Lakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia. Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia. “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: Mtu yeyote anaposikia neno la ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia. Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na hulipokea mara moja kwa furaha. Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye anarudi nyuma mara moja. Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu anayelisikia neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.” Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea. “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’ “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’ “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayangʼoe?’ “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyangʼoe, kwa maana wakati mkingʼoa magugu mnaweza mkangʼoa na ngano pamoja nayo. Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja hadi wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ” Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.”