Malaki 2:1-16
Malaki 2:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu wa majeshi awaambia makuhani: “Sasa enyi makuhani, nawaamuruni hivi: Ni lazima mniheshimu mimi kwa matendo yenu, msiponisikiliza nitawaleteeni laana, vitu vyote mnavyopewa kwa mahitaji yenu nitavilaani. Na kweli nimekwisha kuvilaani, kwa sababu hamuyatilii maanani maagizo yangu. Tazama, nitawaadhibu watoto wenu na nyinyi wenyewe kutokana na uovu wenu, na kuzipaka nyuso zenu mavi ya wanyama wenu wa tambiko. Nitawafukuza mbali nami. Hivyo mtajua kuwa nimewapeni amri hii ili agano langu na ukoo wa Lawi liwe la kudumu. “Katika agano hilo, niliwaahidi uhai na amani na kwamba wao ni lazima kunicha mimi, nao kwa upande wao walinicha mimi, wakaliogopa jina langu. Mafundisho yao yalikuwa ya kweli na kamwe hawakufundisha uongo. Mimi na wao tulikaa kwa amani. Si kwamba walitenda haki tu, bali waliwafundisha wengine kutotenda maovu. Ni wajibu wa makuhani kuwafundisha watu maarifa ya kweli juu ya Mungu. Watu wawaendee kujifunza matakwa yangu kwao, kwani makuhani ni wajumbe wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. “Bali nyinyi makuhani mmegeuka mkaiacha njia ya haki. Mafundisho yenu yamewaongoza watu wengi katika kutenda mabaya. Mmelivunja agano nililofanya nanyi. Nami pia nitawafanya mdharauliwe na kupuuzwa na Waisraeli, kwa sababu hamkuzifuata njia zangu, na mnapowafundisha watu wangu mnapendelea baadhi yao.” Je, sisi sote si watoto wa baba mmoja? Je, sisi sote hatukuumbwa na Mungu yuleyule? Mbona basi, hatuaminiani sisi kwa sisi, na tunalidharau agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na wazee wetu? Watu wa Yuda wamekosa uaminifu kwa Mungu na kutenda machukizo katika Israeli na mjini Yerusalemu. Wamelitia unajisi hekalu la Mwenyezi-Mungu analolipenda. Tena wameoa wanawake wanaoabudu miungu ya kigeni. Mwenyezi-Mungu na awaondolee mbali watu wanaofanya mambo hayo kutoka miongoni mwa wazawa wa Yakobo. Na kamwe wasishiriki katika kutoa ushuhuda na kuleta tambiko mbele ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Zaidi ya hayo yote, mnaifunika madhabahu ya Mwenyezi-Mungu kwa machozi yenu, mkilia na kuomboleza kwa sababu yeye hazikubali tena tambiko mnazomtolea. Mnauliza, “Mbona sasa hazikubali?” Mwenyezi-Mungu hazikubali kwa sababu anajua wazi kuwa umeivunja ahadi yako kwa mke wa ujana wako. Umekosa uaminifu kwake ingawa uliahidi mbele ya Mungu kwamba ungekuwa mwaminifu kwake. Je, Mungu hakuwafanya nyote wawili muwe mwili mmoja na roho moja? Je, alikusudia nini alipofanya hayo? Yamkini alikusudia tuzae watoto ambao watamcha yeye. Kwa hiyo, hakikisheni kuwa hakuna hata mmoja wenu anayekosa uaminifu kwa mkewe. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema: “Ninachukia talaka. Ninachukia mmoja wenu anapomtendea mkewe ukatili huo. Hakikisheni kwamba hakuna hata mmoja wenu anayekosa uaminifu kwa mkewe.”
Malaki 2:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema BWANA wa majeshi, basi nitawaleteeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni. Angalieni, nitaikemea mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam, mavi ya sadaka zenu; nanyi mtaondolewa pamoja nayo Nanyi mtajua ya kuwa mimi nimewaleteeni amri hii, ili agano langu liwe na Lawi, asema BWANA wa majeshi. Agano langu naye lilikuwa agano la uhai na amani; nami nikampa ili aogope, naye akanicha na kulihofu jina langu. Sheria ya kweli ilikuwa kinywani mwake, wala udhalimu haukuonekana midomoni mwake; alikwenda pamoja nami katika amani na unyofu, na kuwageuza wengi hata wakaacha uovu. Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake; kwa kuwa yeye ni mjumbe wa BWANA wa majeshi. Bali ninyi mmegeuka mkaiacha njia; mmewakwaza watu wengi katika sheria; mmeliharibu agano la Lawi, asema BWANA wa majeshi. Kwa sababu hiyo mimi nami nimewafanya ninyi kuwa kitu cha kudharauliwa, na unyonge, mbele ya watu wote, kama vile ninyi msivyozishika njia zangu, bali mmewapendelea watu katika sheria. Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu? Yuda ametenda kwa hiana, na chukizo limetendeka katika Israeli, na katika Yerusalemu; maana Yuda ameunajisi utakatifu wa BWANA aupendao, naye amemwoa binti ya mungu mgeni. BWANA atamtenga mtu atendaye hayo, yeye aliye macho, na yeye ajibuye, atamtenga na hema za Yakobo, pia atamtenga yeye amtoleaye BWANA wa majeshi dhabihu. Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya BWANA kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, ingawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzawa mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.
Malaki 2:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema BWANA wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni. Angalieni, nitaikemea mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam, mavi ya sadaka zenu; nanyi mtaondolewa pamoja nayo Nanyi mtajua ya kuwa mimi nimewapelekeeni amri hii, ili agano langu liwe na Lawi, asema BWANA wa majeshi. Agano langu naye lilikuwa agano la uhai na amani; nami nikampa ili aogope, naye akaniogopa, akalicha jina langu. Sheria ya kweli ilikuwa kinywani mwake, wala udhalimu haukuonekana midomoni mwake; alikwenda pamoja nami katika amani na unyofu, na kuwageuza wengi hata wakaacha uovu. Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake; kwa kuwa yeye ni mjumbe wa BWANA wa majeshi. Bali ninyi mmegeuka mkaiacha njia; mmewakwaza watu wengi katika sheria; mmeliharibu agano la Lawi, asema BWANA wa majeshi. Kwa sababu hiyo mimi nami nimewafanya ninyi kuwa kitu cha kudharauliwa, na unyonge, mbele ya watu wote, kama vile ninyi msivyozishika njia zangu, bali mmewapendelea watu katika sheria. Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu? Yuda ametenda kwa hiana, na chukizo limetendeka katika Israeli, na katika Yerusalemu; maana Yuda ameunajisi utakatifu wa BWANA aupendao, naye amemwoa binti ya mungu mgeni. BWANA atamtenga mtu atendaye hayo, yeye aliye macho, na yeye ajibuye, atamtenga na hema za Yakobo, pia atamtenga yeye amtoleaye BWANA wa majeshi dhabihu. Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya BWANA kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.
Malaki 2:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Sasa onyo hili ni kwa ajili yenu, enyi makuhani. Kama hamtasikiliza, na kama hamtaki kuielekeza mioyo yenu kuheshimu Jina langu, nitatuma laana juu yenu, nami nitalaani baraka zenu. Naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamkuielekeza mioyo yenu kuniheshimu mimi,” Asema BWANA wa majeshi. “Kwa sababu yenu nitawakatilia mbali wazao wenu. Nitazipaka nyuso zenu kinyesi, hicho kinyesi cha dhabihu zenu. Nanyi mtafukuzwa pamoja nazo mtoke mbele zangu. Nanyi mtajua kuwa nimewapelekea onyo hili ili agano langu na Lawi lipate kuendelea,” asema BWANA wa majeshi. “Agano langu lilikuwa pamoja naye, agano la uhai na amani, nami nilimpa yote, ili aniche na kuniheshimu, naye akaniheshimu na kusimama akilicha Jina langu. Fundisho la kweli lilikuwa kinywani mwake, wala hakuna uongo wowote uliopatikana katika midomo yake. Alitembea nami katika amani na unyofu, naye akawageuza wengi kutoka dhambini. “Kwa maana yapasa midomo ya kuhani kuhifadhi maarifa. Tena kutoka kinywani mwake watu wangepaswa kutafuta mafundisho, kwa sababu yeye ni mjumbe wa BWANA wa majeshi. Lakini mmegeuka mkaiacha njia, na kwa mafundisho yenu mmesababisha wengi kujikwaa. Mmevunja agano na Lawi,” asema BWANA wa majeshi. “Kwa hiyo nimewasababisha ninyi kudharauliwa na kufedheheshwa mbele ya watu wote, kwa sababu hamkufuata njia zangu, bali mmeonesha upendeleo katika mambo ya sheria.” Je, sote hatuna Baba mmoja? Hatukuumbwa na Mungu mmoja? Kwa nini basi tunalinajisi agano la baba zetu kwa kukosa uaminifu kila mmoja kwa mwenzake? Yuda amevunja uaminifu. Jambo la kuchukiza limetendeka katika Israeli na katika Yerusalemu: Yuda amepanajisi mahali patakatifu apendapo BWANA, kwa kuoa binti ya mungu mgeni. Kwa maana kwa mtu yeyote atendaye jambo hili, BWANA na amkatilie mbali kutoka mahema ya Yakobo, hata kama huwa anamletea BWANA wa majeshi sadaka. Kitu kingine mnachokifanya: Mnaifurikisha madhabahu ya BWANA kwa machozi. Mnalia na kuugua kwa sababu yeye haziangalii tena sadaka zenu wala hazikubali kwa furaha kutoka mikononi mwenu. Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu BWANA ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa. Je, BWANA hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake. “Ninachukia kuachana,” asema BWANA, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema BWANA wa majeshi. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.