Malaki 2:1-16
Malaki 2:1-16 NENO
“Sasa onyo hili ni kwa ajili yenu, enyi makuhani. Kama hamtasikiliza, na kama hamtaki kuielekeza mioyo yenu kuheshimu Jina langu, nitatuma laana juu yenu, nami nitalaani baraka zenu. Naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamkuielekeza mioyo yenu kuniheshimu mimi,” Asema BWANA wa majeshi. “Kwa sababu yenu nitawakatilia mbali wazao wenu. Nitazipaka nyuso zenu kinyesi, hicho kinyesi cha dhabihu zenu. Nanyi mtafukuzwa pamoja nazo mtoke mbele zangu. Nanyi mtajua kuwa nimewapelekea onyo hili ili agano langu na Lawi lipate kuendelea,” asema BWANA wa majeshi. “Agano langu lilikuwa pamoja naye, agano la uhai na amani, nami nilimpa yote, ili aniche na kuniheshimu, naye akaniheshimu na kusimama akilicha Jina langu. Fundisho la kweli lilikuwa kinywani mwake, wala hakuna uongo wowote uliopatikana katika midomo yake. Alitembea nami katika amani na unyofu, naye akawageuza wengi kutoka dhambini. “Kwa maana yapasa midomo ya kuhani kuhifadhi maarifa. Tena kutoka kinywani mwake watu wangepaswa kutafuta mafundisho, kwa sababu yeye ni mjumbe wa BWANA wa majeshi. Lakini mmegeuka mkaiacha njia, na kwa mafundisho yenu mmesababisha wengi kujikwaa. Mmevunja agano na Lawi,” asema BWANA wa majeshi. “Kwa hiyo nimewasababisha ninyi kudharauliwa na kufedheheshwa mbele ya watu wote, kwa sababu hamkufuata njia zangu, bali mmeonesha upendeleo katika mambo ya sheria.” Je, sote hatuna Baba mmoja? Hatukuumbwa na Mungu mmoja? Kwa nini basi tunalinajisi agano la baba zetu kwa kukosa uaminifu kila mmoja kwa mwenzake? Yuda amevunja uaminifu. Jambo la kuchukiza limetendeka katika Israeli na katika Yerusalemu: Yuda amepanajisi mahali patakatifu apendapo BWANA, kwa kuoa binti ya mungu mgeni. Kwa maana kwa mtu yeyote atendaye jambo hili, BWANA na amkatilie mbali kutoka mahema ya Yakobo, hata kama huwa anamletea BWANA wa majeshi sadaka. Kitu kingine mnachokifanya: Mnaifurikisha madhabahu ya BWANA kwa machozi. Mnalia na kuugua kwa sababu yeye haziangalii tena sadaka zenu wala hazikubali kwa furaha kutoka mikononi mwenu. Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu BWANA ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa. Je, BWANA hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake. “Ninachukia kuachana,” asema BWANA, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema BWANA wa majeshi. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.