Luka 2:1-52
Luka 2:1-52 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote nchini kote wahesabiwe. Sensa hiyo ilikuwa mara ya kwanza, wakati Kurenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. Basi, wote waliohusika walikwenda kuhesabiwa kila mtu katika mji wake. Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya, na kwa vile alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi, alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yudea, alikozaliwa mfalme Daudi. Alikwenda kuhesabiwa pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mjamzito. Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote. Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.” Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu anaowafadhili!” Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.” Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake. Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji. Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake. Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa. Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana. Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.” Pia walikwenda ili watoe sadaka: Hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana. Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria, Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu, akisema: “Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, umruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu ulioleta, ambao umeutayarisha uonekane na watu wote: Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli.” Baba yake Yesu na mama yake walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.” Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. Saa hiyohiyo, alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na kueleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu. Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, wilayani Galilaya. Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa naye. Wazazi wake walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. Siku ya tatu, walimkuta hekaluni kati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutendea hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.
Luka 2:1-52 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa mtawala wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Yudea mpaka katika mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa ukoo na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo Torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto wa kiume aliye kifungua mimba wa mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii mwanamke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipofikisha umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarudi Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwa nini mnitafute? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Luka 2:1-52 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Luka 2:1-52 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Rumi. (Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Siria.) Kila mtu alienda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa. Hivyo Yusufu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Yudea, hadi Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. Alienda huko kujiandikisha pamoja na Mariamu, aliyekuwa amemposa, na alikuwa mjamzito. Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu wa kujifungua ukawa umetimia, naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori la kulia ngʼombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni. Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama, nawaletea habari njema ya furaha itakayokuwa kwa watu wote. Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo, Bwana. Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori la kulia ngʼombe.” Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema, “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.” Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Mariamu na Yusufu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe. Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. Lakini Mariamu akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona. Hata zilipotimia siku nane, uliokuwa wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilopewa na malaika kabla hajatungwa mimba. Ulipotimia wakati wa utakaso wake Mariamu kwa mujibu wa Sheria ya Musa, basi Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda wawili wa njiwa”. Basi huko Yerusalemu kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simeoni, aliyekuwa mwenye haki na mcha Mungu. Alikuwa akitazamia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alienda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema: “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi, sasa mruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako, ulioweka tayari machoni pa watu wote, nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.” Naye Yusufu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.” Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na nne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu. Yusufu na Mariamu walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya. Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akijawa na hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Kila mwaka Yusufu na Mariamu mama yake Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na mbili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yusufu na Mariamu mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Yesu alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua. Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na rafiki zao. Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta. Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa. Yusufu na Mariamu mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.” Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia. Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote. Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.