Yohane 15:1-8
Yohane 15:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda yeye huliondoa, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. Nyinyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. “Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami nikiwa ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote. Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue. Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa. Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu.
Yohane 15:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi hamuwezi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno lolote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
Yohane 15:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
Yohane 15:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi linalozaa, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda. “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, huyo hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa kwa vile mnavyozaa matunda mengi, nanyi mtajidhihirisha kuwa wanafunzi wangu.