Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 6:8-30

Yeremia 6:8-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Hilo na liwe onyo kwako ee Yerusalemu, la sivyo nitakutupa kabisa kwa chuki; nikakufanya uwe jangwa, mahali pasipokaliwa na mtu.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kusanyeni watu wote wa Israeli waliobaki kama watu wakusanyavyo zabibu zote; kama afanyavyo mchumazabibu, pitisheni tena mikono yenu katika matawi yake.” Nitaongea na nani nipate kumwonya, ili wapate kunisikia? Tazama, masikio yao yameziba, hawawezi kusikia ujumbe wako. Kwao neno lako, ee Mwenyezi-Mungu, limekuwa jambo la dhihaka, hawalifurahii hata kidogo. Nimejaa hasira ya Mwenyezi-Mungu dhidi yao. Nashindwa kuizuia ndani yangu. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Imwage hasira barabarani juu ya watoto na pia juu ya makundi ya vijana; wote, mume na mke watachukuliwa, kadhalika na wazee na wakongwe. Nyumba zao zitapewa watu wengine, kadhalika na mashamba yao na wake zao; maana nitaunyosha mkono wangu, kuwaadhibu wakazi wa nchi hii. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wote, tangu mdogo hadi mkubwa kabisa, kila mmoja anatamani kupata faida isiyo halali. Tangu manabii hadi makuhani, kila mmoja wao ni mdanganyifu. Wameliponya jeraha la watu wangu juujuu, wanasema; ‘Amani, amani’, kumbe hakuna amani yoyote! Je, waliona aibu walipofanya machukizo hayo? La! Hawakuona aibu hata kidogo. Hawakujua hata namna ya kuona aibu. Kwa hiyo wataanguka pamoja na wale waangukao; wakati nitakapowaadhibu, wataangamizwa kabisa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Simameni katika njia panda, mtazame. Ulizeni mjue juu ya matukio ya zamani. Tafuteni mahali ilipo njia nzuri muifuate nanyi mtapumzisha nafsi zenu. Lakini wao wakasema: ‘Hatutafuata njia hiyo.’ Kisha nikawawekea walinzi, nikawaambia: ‘Sikilizeni ishara ya tarumbeta.’ Lakini wao wakasema: ‘Hatutaisikiliza.’ “Kwa hiyo, sikilizeni enyi mataifa; enyi jumuiya ya watu jueni yatakayowapata. Sikiliza ee dunia! Mimi nitawaletea maafa watu hawa kulingana na nia zao mbaya. Maana hawakuyajali maneno yangu, na mafundisho yangu nayo wameyakataa. Ya nini kuniletea ubani kutoka Sheba, na udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliki, wala tambiko zenu hazinipendezi. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tazama, nitawawekea watu hawa vikwazo ambavyo vitawakwaza na kuwaangusha chini. Akina baba na watoto wao wa kiume wataangamia, kadhalika na majirani na marafiki.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Tazameni, watu wanakuja toka nchi ya kaskazini; taifa kubwa linajitayarisha kutoka mbali duniani. Wamezishika pinde zao na mikuki, watu wakatili wasio na huruma. Vishindo vyao ni kama ngurumo ya bahari. Wamepanda farasi, wamejipanga tayari kwa vita, dhidi yako ewe Siyoni!” Waisraeli wanasema, “Tumesikia habari zao, mikono yetu imelegea; tumeshikwa na dhiki na uchungu, kama mwanamke anayejifungua. Hatuwezi kwenda mashambani, wala kutembea barabarani; maadui wameshika silaha mikononi, vitisho vimejaa kila mahali.” Mwenyezi-Mungu asema, “Jivikeni mavazi ya gunia, enyi watu wangu na kugaagaa katika majivu. Ombolezeni kwa uchungu, kama mtu anayemwombolezea mwana wa pekee, maana mwangamizi atakuja, na kuwashambulia ghafla. Yeremia, wewe nimekuweka kuwa mchunguzi na mpimaji wa watu wangu, ili uchunguze na kuzijua njia zao. Wote ni waasi wakaidi, ni watu wanaopitapita wakisengenya wengine, wagumu kama shaba nyeusi au chuma; wote hutenda kwa ufisadi. Mifuo inafukuta kwa nguvu, risasi inayeyukia humohumo motoni; ni bure kuendelea kuwatakasa watu wangu, waovu hawawezi kuondolewa uchafu wao. Wataitwa ‘Takataka za fedha’, maana mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa.”

Shirikisha
Soma Yeremia 6

Yeremia 6:8-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Uonyeke, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu. BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu. Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la BWANA limekuwa matukano kwao; hawalifurahii. Lakini nimejaa ghadhabu ya BWANA; nimechoka kwa kujizuia; imwageni juu ya watoto walio njiani, na juu ya kusanyiko la vijana pia; maana hata mume atatwaliwa pamoja na mkewe, mzee pamoja na yeye aliyetimiza siku zake. Na nyumba zao zitakuwa mali za watu wengine, mashamba yao na wake zao pamoja; kwa kuwa nitaunyosha mkono wangu juu ya wenyeji wa nchi hii, asema BWANA. Kwa maana, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa miongoni mwao, kila mmoja ni mtamanifu; na, tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu. Wameliponya jeraha la watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani. Je! Walitahayarika, walipokuwa wameunda machukizo? La, hawakutahayarika hata kidogo, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi, wataanguka miongoni mwa hao waangukao; wakati nitakapowajia wataangushwa chini, asema BWANA. BWANA asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, Iko wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo. Nami niliweka walinzi juu yenu, wakisema, Isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema, Hatutaki kusikiliza. Kwa sababu hiyo sikilizeni, enyi mataifa, mkajue, Ee kusanyiko, ni jambo gani litokealo kati yao. Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa. Yafaa nini niletewe ubani kutoka Sheba, na udi kutoka nchi iliyo mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliwi, wala dhabihu zenu haziniridhii. Basi, kwa hiyo, BWANA asema hivi, Tazama, nitaweka makwazo mbele ya watu hawa, na baba na wana wao watajikwaa pamoja; jirani ya mtu na rafiki yake watapotea. BWANA asema hivi, Tazama, watu wanakuja, wakitoka katika nchi ya kaskazini; na taifa kubwa litaamshwa, litokalo katika pande za mwisho wa dunia. Washika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao huvuma kama bahari, nao wamepanda farasi wao; kila mmoja kama mtu wa vita amejipanga juu yako, Ee binti Sayuni. Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na uchungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake. Msitoke kwenda mashambani, wala msitembee njiani, kwa maana upanga wa adui uko huko; hofu ziko pande zote. Ee binti wa watu wangu, ujivike nguo ya magunia, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafla. Nimekuweka uwe mnara na ngome kati ya watu wangu; upate kuijua njia yao na kuijaribu. Ni waasi kupita kiasi wote pia, waendao huku na huko wakisingizia, ni shaba na chuma hao, hutenda dhuluma wote pia. Mifuo inafukuta kwa nguvu; risasi tu inatoka katika moto huo; mfua fedha ameyeyusha bure tu; maana wabaya hawaondolewi mbali. Watu watawaita taka za fedha, kwa sababu BWANA amewakataa.

Shirikisha
Soma Yeremia 6

Yeremia 6:8-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Uadhibishwe, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu. BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu. Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la BWANA limekuwa matukano kwao; hawalifurahii. Lakini nimejaa ghadhabu ya BWANA; nimechoka kwa kujizuia; imwageni juu ya watoto walio njiani, na juu ya kusanyiko la vijana pia; maana hata mume atatwaliwa pamoja na mkewe, mzee pamoja na yeye aliyetimiza siku zake. Na nyumba zao zitakuwa mali za watu wengine, mashamba yao na wake zao pamoja; kwa kuwa nitaunyosha mkono wangu juu ya wenyeji wa nchi hii, asema BWANA. Kwa maana, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa miongoni mwao, kila mmoja ni mtamanifu; na, tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu. Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani. Je! Walitahayarika, walipokuwa wameunda machukizo? La, hawakutahayarika hata kidogo, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi, wataanguka miongoni mwa hao waangukao; wakati nitakapowajilia wataangushwa chini, asema BWANA. BWANA asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo. Nami naliweka walinzi juu yenu, wakisema, Isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema, Hatutaki kusikiliza. Kwa sababu hiyo sikilizeni, enyi mataifa, mkajue, Ee kusanyiko, ni jambo gani litokealo kati yao. Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa. Yafaa nini niletewe ubani kutoka Sheba, na uudi kutoka nchi iliyo mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliwi, wala dhabihu zenu haziniridhii. Basi, kwa hiyo, BWANA asema hivi, Tazama, nitaweka makwazo mbele ya watu hawa, na baba na wana wao watajikwaa pamoja; jirani ya mtu na rafiki yake watapotea. BWANA asema hivi, Tazama, watu wanakuja, wakitoka katika nchi ya kaskazini; na taifa kubwa litaamshwa, litokalo katika pande za mwisho wa dunia. Washika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao huvuma kama bahari, nao wamepanda farasi zao; kila mmoja kama mtu wa vita amejipanga juu yako, Ee binti Sayuni. Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake. Msitoke kwenda mashambani, wala msitembee njiani, kwa maana upanga wa adui uko huko; hofu ziko pande zote. Ee binti wa watu wangu, ujivike nguo ya magunia, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafula. Nimekuweka uwe mnara na ngome kati ya watu wangu; upate kuijua njia yao na kuijaribu. Ni waasi kupita kiasi wote pia, waendao huko na huko wakisingizia, ni shaba na chuma hao, hutenda dhuluma wote pia. Mifuo inafukuta kwa nguvu; risasi tu inatoka katika moto huo; mfua fedha ameyeyusha bure tu; maana wabaya hawaondolewi mbali. Watu watawaita taka za fedha, kwa sababu BWANA amewakataa.

Shirikisha
Soma Yeremia 6

Yeremia 6:8-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Pokea onyo, ee Yerusalemu, la sivyo nitageukia mbali nawe na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa, asiweze mtu kuishi ndani yake.” Hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi: “Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli kwa uangalifu kama kwenye mzabibu; pitisha mkono wako kwenye matawi tena, kama yeye avunaye zabibu.” Niseme na nani na kumpa onyo? Ni nani atakayenisikiliza mimi? Masikio yao yameziba, kwa hiyo hawawezi kusikia. Neno la BWANA ni chukizo kwao, hawalifurahii. Lakini nimejaa ghadhabu ya BWANA, nami siwezi kuizuia. “Wamwagie watoto walio barabarani, na juu ya vijana wa kiume waliokusanyika; mume na mke watakumbwa pamoja ndani yake, hata nao wazee waliolemewa na miaka. Nyumba zao zitapewa watu wengine, pamoja na mashamba yao na wake zao, nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya wale wanaoishi katika nchi,” asema BWANA. “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata faida zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. Wanafunga majeraha ya watu wangu bila uangalifu. Wanasema, ‘Amani, amani,’ wakati hakuna amani. Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno? Hapana, hawana haya hata kidogo; hawajui hata kuona aibu. Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka, watashushwa chini nitakapowaadhibu,” asema BWANA. Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Simama kwenye njia panda utazame, ulizia mapito ya zamani, ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo, nanyi mtapata amani nafsini mwenu. Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita njia hiyo.’ Niliweka walinzi juu yenu na kusema, ‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’ Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’ Kwa hiyo sikilizeni, enyi mataifa, angalieni, enyi mashahidi, lile litakalowatokea. Sikia, ee nchi: Ninaleta maafa juu ya watu hawa, matunda ya mipango yao, kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu na wameikataa sheria yangu. Unanifaa nini uvumba kutoka Sheba, au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali? Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki, dhabihu zako hazinifurahishi mimi.” Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Nitaweka vikwazo mbele ya watu hawa. Baba na wana wao watajikwaa juu yake, majirani na rafiki wataangamia.” Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Tazama, jeshi linakuja kutoka nchi ya kaskazini, taifa kubwa linaamshwa kutoka miisho ya dunia. Wamejifunga pinde na mkuki, ni wakatili na hawana huruma. Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma wanapoendesha farasi wao. Wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita ili kukushambulia, ee Binti Sayuni.” Tumesikia taarifa zao, nayo mikono yetu imelegea. Uchungu umetushika, maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa. Usitoke kwenda mashambani au kutembea barabarani, kwa kuwa adui ana upanga, na kuna vitisho kila upande. Enyi watu wangu, vaeni magunia mjivingirishe kwenye majivu, ombolezeni kwa kilio cha uchungu kama amliliaye mwana pekee, kwa maana ghafula mharibu atatujia. “Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma, nao watu wangu kama mawe yenye madini, ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao. Wote ni waasi sugu, wakienda huku na huko kusengenya. Wao ni shaba na chuma, wote wanatenda upotovu. Mivuo inavuma kwa nguvu, kinachoungua kwa huo moto ni risasi, lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure; waovu hawaondolewi. Wanaitwa fedha iliyokataliwa, kwa sababu BWANA amewakataa.”

Shirikisha
Soma Yeremia 6