Yeremia 6:8-30
Yeremia 6:8-30 NENO
Pokea onyo, ee Yerusalemu, la sivyo nitageukia mbali nawe na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa, asiweze mtu kuishi ndani yake.” Hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi: “Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli kwa uangalifu kama kwenye mzabibu; pitisha mkono wako kwenye matawi tena, kama yeye avunaye zabibu.” Niseme na nani na kumpa onyo? Ni nani atakayenisikiliza mimi? Masikio yao yameziba, kwa hiyo hawawezi kusikia. Neno la BWANA ni chukizo kwao, hawalifurahii. Lakini nimejaa ghadhabu ya BWANA, nami siwezi kuizuia. “Wamwagie watoto walio barabarani, na juu ya vijana wa kiume waliokusanyika; mume na mke watakumbwa pamoja ndani yake, hata nao wazee waliolemewa na miaka. Nyumba zao zitapewa watu wengine, pamoja na mashamba yao na wake zao, nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya wale wanaoishi katika nchi,” asema BWANA. “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata faida zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. Wanafunga majeraha ya watu wangu bila uangalifu. Wanasema, ‘Amani, amani,’ wakati hakuna amani. Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno? Hapana, hawana haya hata kidogo; hawajui hata kuona aibu. Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka, watashushwa chini nitakapowaadhibu,” asema BWANA. Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Simama kwenye njia panda utazame, ulizia mapito ya zamani, ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo, nanyi mtapata amani nafsini mwenu. Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita njia hiyo.’ Niliweka walinzi juu yenu na kusema, ‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’ Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’ Kwa hiyo sikilizeni, enyi mataifa, angalieni, enyi mashahidi, lile litakalowatokea. Sikia, ee nchi: Ninaleta maafa juu ya watu hawa, matunda ya mipango yao, kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu na wameikataa sheria yangu. Unanifaa nini uvumba kutoka Sheba, au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali? Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki, dhabihu zako hazinifurahishi mimi.” Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Nitaweka vikwazo mbele ya watu hawa. Baba na wana wao watajikwaa juu yake, majirani na rafiki wataangamia.” Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Tazama, jeshi linakuja kutoka nchi ya kaskazini, taifa kubwa linaamshwa kutoka miisho ya dunia. Wamejifunga pinde na mkuki, ni wakatili na hawana huruma. Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma wanapoendesha farasi wao. Wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita ili kukushambulia, ee Binti Sayuni.” Tumesikia taarifa zao, nayo mikono yetu imelegea. Uchungu umetushika, maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa. Usitoke kwenda mashambani au kutembea barabarani, kwa kuwa adui ana upanga, na kuna vitisho kila upande. Enyi watu wangu, vaeni magunia mjivingirishe kwenye majivu, ombolezeni kwa kilio cha uchungu kama amliliaye mwana pekee, kwa maana ghafula mharibu atatujia. “Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma, nao watu wangu kama mawe yenye madini, ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao. Wote ni waasi sugu, wakienda huku na huko kusengenya. Wao ni shaba na chuma, wote wanatenda upotovu. Mivuo inavuma kwa nguvu, kinachoungua kwa huo moto ni risasi, lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure; waovu hawaondolewi. Wanaitwa fedha iliyokataliwa, kwa sababu BWANA amewakataa.”