Yeremia 4:1-9
Yeremia 4:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ukitaka kurudi ee Israeli, nirudie mimi. Ukiviondoa vitu vya kuchukiza mbele yangu, usipotangatanga huko na huko, ukiapa kwa ukweli, unyofu na uadilifu, kwa kusema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo’, ndipo mataifa yatakapopata baraka kwangu, na kutukuka kwa sababu yangu.” Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu: “Limeni mashamba yenu mapya; msipande mbegu zenu penye miiba. Enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, jitakaseni kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu, wekeni mioyo yenu wazi mbele yangu. La sivyo, ghadhabu yangu itachomoza kama moto, iwake hata pasiwe na mtu wa kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu. “Tangazeni huko Yuda, pazeni sauti huko Yerusalemu! Pigeni tarumbeta kila mahali nchini! Pazeni sauti na kusema: Kusanyikeni pamoja! Kimbilieni miji yenye ngome! Twekeni bendera ya vita kuelekea Siyoni, kimbilieni usalama wenu, msisitesite! Mwenyezi-Mungu analeta maafa na maangamizi makubwa kutoka kaskazini. Kama simba atokavyo mafichoni mwake, mwangamizi wa mataifa ameanza kuja, anakuja kutoka mahali pake, ili kuiharibu nchi yako. Miji yako itakuwa magofu matupu, bila kukaliwa na mtu yeyote. Kwa hiyo, vaa vazi la gunia, omboleza na kulia; maana, hasira kali ya Mwenyezi-Mungu, bado haijaondoka kwetu. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Siku hiyo, mfalme na wakuu watakufa moyo; makuhani watapigwa na bumbuazi, na manabii watashangaa.”
Yeremia 4:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kama ukitaka kurudi, Ee Israeli, asema BWANA, utanirudia mimi; na kama ukitaka kuyaondoa machukizo yako, yasiwe mbele ya macho yangu, ndipo hutaondolewa; nawe utaapa hivi, Kama BWANA aishivyo, katika kweli, na katika hukumu, na katika haki ndipo mataifa watabarikiwa na yeye, nao watajitukuza katika yeye. Maana BWANA awaambia hivi watu wa Yuda na Yerusalemu Ulimeni udongo katika konde zenu, wala msipande mbegu kati ya miiba. Jitahirini kwa BWANA, mkayaondoe magovi ya mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu. Tangazeni katika Yuda, hubirini katika Yerusalemu, na kusema, Pigeni baragumu katika nchi, pigeni kelele sana, na kusema, Jikusanyeni pamoja, tukaingie katika miji yenye boma. Twekeni bendera kuelekea Sayuni; kimbieni mpate kuwa salama, msikawie; kwa maana nitaleta mabaya toka kaskazini, na maangamizi makuu. Simba ametoka katika kichaka chake, ndiye aangamizaye mataifa; ameanza kushika njia, ametoka katika mahali pake; ili aifanye nchi yako kuwa ukiwa, miji yako ifanywe maganjo, asibaki mwenyeji ndani yake. Kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya BWANA haikugeuka na kutuacha. Na katika siku hiyo itakuwa, asema BWANA, moyo wa mfalme utapotea, na moyo wa wakuu wake; na makuhani watastaajabu, na manabii watashangaa.
Yeremia 4:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kama ukitaka kurudi, Ee Israeli, asema BWANA, utanirudia mimi; na kama ukitaka kuyaondoa machukizo yako, yasiwe mbele ya macho yangu, ndipo hutaondolewa; nawe utaapa hivi, Kama BWANA aishivyo, katika kweli, na katika hukumu, na katika haki ndipo mataifa watajibariki katika yeye, nao watajitukuza katika yeye. Maana BWANA awaambia hivi watu wa Yuda na Yerusalemu Ulimeni udongo katika konde zenu, wala msipande mbegu kati ya miiba. Jitahirini kwa BWANA, mkaziondoe govi za mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu. Tangazeni katika Yuda, hubirini katika Yerusalemu, na kusema, Pigeni baragumu katika nchi, pigeni kelele sana, na kusema, Jikusanyeni pamoja, tukaingie katika miji yenye boma. Twekeni bendera kuelekea Sayuni; kimbieni mpate kuwa salama, msikawie; kwa maana nitaleta mabaya toka kaskazini, na maangamivu makuu. Simba ametoka katika kichaka chake, ndiye aangamizaye mataifa; ameanza kushika njia, ametoka katika mahali pake; ili aifanye nchi yako kuwa ukiwa, miji yako ifanywe maganjo, asibaki mwenyeji ndani yake. Kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya BWANA haikugeuka na kutuacha. Na katika siku hiyo itakuwa, asema BWANA, moyo wa mfalme utapotea, na moyo wa wakuu wake; na makuhani watastaajabu, na manabii watashangaa.
Yeremia 4:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli, nirudie mimi,” asema BWANA. “Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu na usiendelee kutangatanga, ikiwa utaapa katika kweli, kwa haki na kwa unyofu, ‘Hakika kama BWANA aishivyo,’ ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye, na ndani yake watajitukuza.” Hili ndilo asemalo BWANA kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu: “Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu, wala msipande katikati ya miiba. Jitahirini katika BWANA, tahirini mioyo yenu, enyi wanaume wa Yuda na watu wa Yerusalemu, la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu na kuwaka kama moto kwa sababu ya uovu mliotenda, ikiwaka pasipo wa kuizima. “Tangaza katika Yuda na upige mbiu katika Yerusalemu, useme: ‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’ Piga kelele na kusema: ‘Kusanyikeni pamoja! Tukimbilie katika miji yenye ngome!’ Inueni ishara ili kwenda Sayuni! Kimbilieni usalama pasipo kuchelewa! Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini, maangamizi ya kutisha.” Simba ametoka nje ya pango lake, mwangamizi wa mataifa amejipanga. Ametoka mahali pake ili aangamize nchi yenu. Miji yenu itakuwa magofu pasipo mtu wa kuishi humo. Hivyo vaeni magunia, ombolezeni na kulia kwa huzuni, kwa kuwa hasira kali ya BWANA haijaondolewa kwetu. “Katika siku ile,” asema BWANA “mfalme na maafisa watakata tamaa, makuhani watafadhaika, na manabii watashangazwa mno.”