Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 2:1-30

Yeremia 2:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Nenda ukawatangazie waziwazi wakazi wote wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Naukumbuka uaminifu wako ulipokuwa kijana, jinsi ulivyonipenda kama mchumba wako, ulivyonifuata jangwani kwenye nchi ambayo haikupandwa kitu. Israeli, wewe ulikuwa mtakatifu kwangu, ulikuwa matunda ya kwanza ya mavuno yangu. Wote waliokudhuru walikuwa na hatia, wakapatwa na maafa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Yakobo. Sikilizeni enyi jamaa zote za wazawa wa Israeli. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wazee wenu waliona kosa gani kwangu hata wakanigeuka na kuniacha, wakakimbilia miungu duni, hata nao wakawa watu duni? Hawakujiuliza: ‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu aliyetutoa nchini Misri, aliyetuongoza nyikani katika nchi ya jangwa na makorongo, nchi kame na yenye giza nene, nchi isiyopitiwa na mtu yeyote, wala kukaliwa na binadamu?’ Niliwaleta katika nchi yenye rutuba, muyafurahie mazao yake na mema yake mengine. Lakini mlipofika tu mliichafua nchi yangu, mkaifanya chukizo nchi niliyowapa iwe yenu. Nao makuhani hawakujiuliza: ‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu?’ Wataalamu wa sheria hawakunijua, viongozi wa watu waliniasi; manabii nao walitabiri kwa jina la Baali na kuabudu sanamu zisizo na faida yoyote.” Mwenyezi-Mungu asema, “Kwa hiyo, mimi nitawalaumu nyinyi, na nitawalaumu wazawa wenu. Haya, vukeni bahari hadi Kupro mkaone, au tumeni watu huko Kedari wakachunguze, kama jambo kama hili limewahi kutokea: Kwamba kuna taifa lililowahi kubadilisha miungu yake ingawa miungu hiyo si miungu! Lakini watu wangu wameniacha mimi, utukufu wao, wakafuata miungu isiyofaa kitu. Shangaeni enyi mbingu, juu ya jambo hili, mkastaajabu na kufadhaika kabisa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Maana, watu wangu wametenda maovu mawili; wameniacha mimi niliye chemchemi ya maji ya uhai, wakajichimbia visima vyao wenyewe, visima vyenye nyufa, visivyoweza kuhifadhi maji. “Je, Israeli ni mtumwa, ama amezaliwa utumwani? Mbona basi amekuwa kama mawindo? Simba wanamngurumia, wananguruma kwa sauti kubwa. Nchi yake wameifanya jangwa, miji yake imekuwa magofu, haina watu. Isitoshe, watu wa Memfisi na Tahpanesi, wameuvunja utosi wake. Israeli, je, hayo yote si umejiletea mwenyewe, kwa kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekuwa ninakuongoza njiani? Na sasa itakufaa nini kwenda Misri, kunywa maji ya mto Nili? Au itakufaa nini kwenda Ashuru, kunywa maji ya mto Eufrate? Uovu wako utakuadhibu; na uasi wako utakuhukumu. Ujue na kutambua kuwa ni vibaya mno kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuondoa uchaji wangu ndani yako. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. “Tangu zamani wewe ulivunja nira yako, ukaikatilia mbali minyororo yako, ukasema, ‘Sitakutumikia’. Juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wa majani mabichi, uliinamia miungu ya rutuba kama kahaba. Lakini mimi nilikupanda kama mzabibu mteule, mzabibu wenye afya na wa mbegu safi; mbona basi umeharibika, ukageuka kuwa mzabibu mwitu? Hata ukijiosha kwa magadi, na kutumia sabuni nyingi, madoa ya uovu wako bado yatabaki mbele yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Unawezaje kusema, ‘Mimi si najisi; sijawafuata Mabaali?’ Tazama ulivyotenda dhambi kule bondeni; angalia ulivyofanya huko! Wewe ni kama mtamba wa ngamia, akimbiaye huko na huko; kama pundamwitu aliyezoea jangwani. Katika tamaa yake hunusanusa upepo; nani awezaye kuizuia hamu yake? Amtakaye hana haja ya kujisumbua; wakati wake ufikapo watampata tu. Israeli, usiichakaze miguu yako wala usilikaushe koo lako. Lakini wewe wasema: ‘Hakuna tumaini lolote. Nimeipenda miungu ya kigeni, hiyo ndiyo nitakayoifuata.’ “Kama vile mwizi aonavyo aibu akishikwa, ndivyo Waisraeli watakavyoona aibu; wao wenyewe, wafalme wao, wakuu wao, makuhani wao na manabii wao. Hao huuambia mti: ‘Wewe u baba yangu,’ na jiwe: ‘Wewe ndiwe uliyenizaa;’ kwa maana wamenipa kisogo, wala hawakunielekezea nyuso zao. Lakini wakati wa shida husema: ‘Inuka utuokoe!’ “Lakini iko wapi miungu yako uliyojifanyia? Iinuke basi, kama inaweza kukusaidia, wakati unapokuwa katika shida. Ee Yuda, idadi ya miungu yako ni sawa na idadi ya miji yako! Mbona mnanilalamikia? Nyinyi nyote mmeniasi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Niliwaadhibu watu wako bila kufanikiwa, wao wenyewe walikataa kukosolewa. Upanga wako uliwamaliza manabii wako kama simba mwenye uchu.

Shirikisha
Soma Yeremia 2

Yeremia 2:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno la BWANA likanijia, kusema, Nenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Nakukumbuka, hisani ya ujana wako, upendo wa wakati wa kuposwa kwako; Jinsi ulivyonifuata huko jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu. Israeli walikuwa utakatifu kwa BWANA; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajia; asema BWANA. Lisikieni neno la BWANA, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli. BWANA asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili? Wala hawakusema, Yuko wapi BWANA, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu? Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo. Makuhani hawakusema, Yuko wapi BWANA? Wala wanasheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu. Basi, kwa ajili ya hayo nitateta nanyi, asema BWANA, nami nitateta na watoto wa watoto wenu. Maana, vukeni mpaka visiwa vya Kitimu, mkaone; tumeni watu waende Kedari, mkafikiri sana; mkaone kwamba jambo kama hili limekuwa wakati wowote. Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia. Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema BWANA. Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia visima, visima vyenye nyufa visivyoweza kuweka maji. Je! Israeli ni mtumwa? Je! Ni mzalia? Mbona amekuwa mateka? Wanasimba wamenguruma juu yake, wametoa sana sauti zao; Nao wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketea, haina watu. Tena wana wa Nofu na Tapanesi wamevunja utosi wa kichwa chako. Je! Hukujipatia mambo haya mwenyewe, kwa kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, alipokuongoza njiani? Na sasa una nini utakayofaidi katika njia iendayo Misri, kunywa maji ya Shihori? Au una nini utakayofaidi katika njia iendayo Ashuru, kunywa maji ya ule Mto? Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, BWANA wa majeshi. Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. Nami nilikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibumwitu machoni pangu? Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU. Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake; punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichosha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona. Zuia mguu wako usikose kiatu, na koo yako isiwe na kiu; lakini wewe ulisema, Hakuna matumaini kabisa; la, maana nimewapenda wageni, nami nitawafuata. Kama mwizi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao; waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe. Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda. Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema BWANA. Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye.

Shirikisha
Soma Yeremia 2

Yeremia 2:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno la BWANA likanijia, kusema, Enenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Nakukumbuka, hisani ya ujana wako, upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuata huko jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu. Israeli walikuwa utakatifu kwa BWANA; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajilia; asema BWANA. Lisikieni neno la BWANA, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli. BWANA asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili? Wala hawakusema, Yuko wapi BWANA, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu? Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo. Makuhani hawakusema, Yuko wapi BWANA? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu. Basi, kwa ajili ya hayo nitateta nanyi, asema BWANA, nami nitateta na watoto wa watoto wenu. Maana, vukeni mpaka visiwa vya Kitimu, mkaone; tumeni watu waende Kedari, mkafikiri sana; mkaone kwamba jambo kama hili limekuwa wakati wo wote. Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia. Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema BWANA. Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji. Je! Israeli ni mtumwa? Je! Ni mzalia? mbona amekuwa mateka? Wana-simba wamenguruma juu yake, wametoa sana sauti zao; Nao wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketea, haina watu. Tena wana wa Nofu na Tahpanesi wamevunja utosi wa kichwa chako. Je! Hukujipatia mambo haya mwenyewe, kwa kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, alipokuongoza njiani? Na sasa una nini utakayotenda katika njia iendayo Misri, kunywa maji ya Shihori? Au una nini utakayotenda katika njia iendayo Ashuru, kunywa maji ya ule Mto? Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, BWANA wa majeshi. Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu? Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU. Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake; punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichokesha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona. Zuia mguu wako usikose kiatu, na koo yako isiwe na kiu; lakini wewe ulisema, Hapana matumaini kabisa; la, maana nimewapenda wageni, nami nitawafuata. Kama mwivi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao; waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe. Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda. Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema BWANA. Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye.

Shirikisha
Soma Yeremia 2

Yeremia 2:1-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Neno la BWANA lilinijia kusema, “Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu: “Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako, jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi na kunifuata katika jangwa lile lote, katika nchi isiyopandwa mbegu. Israeli alikuwa mtakatifu kwa BWANA, kama malimbuko ya kwanza ya mavuno yake; wote waliomwangamiza walihesabiwa kuwa na hatia, nayo maafa yaliwakumba,’ ” asema BWANA. Sikia neno la BWANA, ee nyumba ya Yakobo, nanyi nyote jamaa za nyumba ya Israeli. Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu, hata wakatangatanga mbali nami hivyo? Walifuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili. Hawakuuliza, ‘Yuko wapi BWANA, aliyetupandisha kutoka Misri na kutuongoza kupitia nyika kame, kupitia nchi ya majangwa na mabonde, nchi ya ukame na giza, nchi ambayo hakuna mtu asafiriye ndani yake wala hakuna mtu aishiye humo?’ Niliwaleta katika nchi yenye wingi wa vitu ili mpate kula matunda yake na utajiri wa mazao yake. Lakini mkaja na kuinajisi nchi yangu, na kuufanya urithi wangu chukizo. Makuhani hawakuuliza, ‘Yuko wapi BWANA?’ Wale wanaoshughulikia sheria hawakunijua mimi; viongozi waliasi dhidi yangu. Manabii walitabiri kwa jina la Baali, wakifuata sanamu batili. “Kwa hiyo naleta tena mashtaka dhidi yako,” asema BWANA. “Nami nitaleta mashtaka dhidi ya watoto wa watoto wako. Vuka, nenda ngʼambo hadi pwani ya Kitimu nawe uangalie, tuma watu waende Kedari, wachunguze kwa makini, uone kama kumeshawahi kuwa kitu kama hiki. Je, taifa limebadili miungu yake wakati wowote? (Hata ingawa hao si miungu kamwe.) Lakini watu wangu wamebadili Utukufu wao kwa sanamu batili. Shangaeni katika hili, ee mbingu, nanyi tetemekeni kwa hofu kuu,” asema BWANA. “Watu wangu wametenda dhambi mbili: Wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji yaliyo hai, nao wamejichimbia visima vyao wenyewe, visima vilivyobomoka, visivyoweza kuhifadhi maji. Je, Israeli ni mtumishi, yaani mtumwa kwa kuzaliwa? Kwa nini basi amekuwa mateka? Simba wamenguruma; wamemngurumia. Wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketezwa, nayo imeachwa haina watu. Pia watu wa Memfisi na Tapanesi wamekupiga fuvu la kichwa. Je, hukujiletea hili wewe mwenyewe kwa kumwacha BWANA, Mungu wako alipowaongoza njiani? Sasa kwa nini uende Misri kunywa maji ya Shihori? Nawe kwa nini kwenda Ashuru kunywa maji ya Mto? Uovu wako utakuadhibu; kurudi nyuma kwako kutakukemea. Basi kumbuka, utambue jinsi lilivyo jambo ovu na chungu kwako unapomwacha BWANA Mungu wako, na kutokuwa na hofu yangu,” asema Bwana, BWANA wa majeshi. “Zamani nilivunja nira yako na kukatilia mbali vifungo vyako; ukasema, ‘Sitakutumikia!’ Hakika, kwenye kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda matawi yake ulijilaza kama kahaba. Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana, mkamilifu na wa mbegu nzuri. Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami, ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu? Hata ujisafishe kwa magadi na kutumia sabuni nyingi, bado doa la hatia yako liko mbele zangu,” asema BWANA Mwenyezi. “Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi, sijawafuata Mabaali’? Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni; fikiri uliyoyafanya. Wewe ni ngamia jike mwenye mbio ukikimbia hapa na pale, punda-mwitu aliyezoea jangwa, anayenusa upepo katika tamaa yake kubwa: wakati wake wa kuhitaji mbegu ni nani awezaye kumzuia? Madume yoyote yanayomfuatilia hayana haja ya kujichosha; wakati wa kupandwa kwake yatampata tu. Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu, na koo lako liwe limekauka. Lakini ulisema, ‘Haina maana! Ninaipenda miungu ya kigeni, nami lazima niifuatie.’ “Kama vile mwizi anavyoaibika akikamatwa, hivyo ndivyo nyumba ya Israeli inavyoaibishwa: wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao. Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’ nalo jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’ Wamenipa visogo vyao wala hawakunigeuzia nyuso zao; lakini wakiwa katika taabu, wanasema, ‘Njoo utuokoe!’ Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea? Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa wakati mko katika taabu! Kwa maana mna miungu mingi kama mlivyo na miji, ee Yuda. “Kwa nini mnaleta mashtaka dhidi yangu? Ninyi nyote mmeniasi,” asema BWANA. “Nimeadhibu watu wako bure tu, hawakujirekebisha. Upanga wako umewala manabii wako kama simba mwenye njaa.

Shirikisha
Soma Yeremia 2