Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 2:1-30

Yeremia 2:1-30 NENO

Neno la BWANA lilinijia kusema, “Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu: “Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako, jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi na kunifuata katika jangwa lile lote, katika nchi isiyopandwa mbegu. Israeli alikuwa mtakatifu kwa BWANA, kama malimbuko ya kwanza ya mavuno yake; wote waliomwangamiza walihesabiwa kuwa na hatia, nayo maafa yaliwakumba,’ ” asema BWANA. Sikia neno la BWANA, ee nyumba ya Yakobo, nanyi nyote jamaa za nyumba ya Israeli. Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu, hata wakatangatanga mbali nami hivyo? Walifuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili. Hawakuuliza, ‘Yuko wapi BWANA, aliyetupandisha kutoka Misri na kutuongoza kupitia nyika kame, kupitia nchi ya majangwa na mabonde, nchi ya ukame na giza, nchi ambayo hakuna mtu asafiriye ndani yake wala hakuna mtu aishiye humo?’ Niliwaleta katika nchi yenye wingi wa vitu ili mpate kula matunda yake na utajiri wa mazao yake. Lakini mkaja na kuinajisi nchi yangu, na kuufanya urithi wangu chukizo. Makuhani hawakuuliza, ‘Yuko wapi BWANA?’ Wale wanaoshughulikia sheria hawakunijua mimi; viongozi waliasi dhidi yangu. Manabii walitabiri kwa jina la Baali, wakifuata sanamu batili. “Kwa hiyo naleta tena mashtaka dhidi yako,” asema BWANA. “Nami nitaleta mashtaka dhidi ya watoto wa watoto wako. Vuka, nenda ngʼambo hadi pwani ya Kitimu nawe uangalie, tuma watu waende Kedari, wachunguze kwa makini, uone kama kumeshawahi kuwa kitu kama hiki. Je, taifa limebadili miungu yake wakati wowote? (Hata ingawa hao si miungu kamwe.) Lakini watu wangu wamebadili Utukufu wao kwa sanamu batili. Shangaeni katika hili, ee mbingu, nanyi tetemekeni kwa hofu kuu,” asema BWANA. “Watu wangu wametenda dhambi mbili: Wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji yaliyo hai, nao wamejichimbia visima vyao wenyewe, visima vilivyobomoka, visivyoweza kuhifadhi maji. Je, Israeli ni mtumishi, yaani mtumwa kwa kuzaliwa? Kwa nini basi amekuwa mateka? Simba wamenguruma; wamemngurumia. Wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketezwa, nayo imeachwa haina watu. Pia watu wa Memfisi na Tapanesi wamekupiga fuvu la kichwa. Je, hukujiletea hili wewe mwenyewe kwa kumwacha BWANA, Mungu wako alipowaongoza njiani? Sasa kwa nini uende Misri kunywa maji ya Shihori? Nawe kwa nini kwenda Ashuru kunywa maji ya Mto? Uovu wako utakuadhibu; kurudi nyuma kwako kutakukemea. Basi kumbuka, utambue jinsi lilivyo jambo ovu na chungu kwako unapomwacha BWANA Mungu wako, na kutokuwa na hofu yangu,” asema Bwana, BWANA wa majeshi. “Zamani nilivunja nira yako na kukatilia mbali vifungo vyako; ukasema, ‘Sitakutumikia!’ Hakika, kwenye kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda matawi yake ulijilaza kama kahaba. Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana, mkamilifu na wa mbegu nzuri. Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami, ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu? Hata ujisafishe kwa magadi na kutumia sabuni nyingi, bado doa la hatia yako liko mbele zangu,” asema BWANA Mwenyezi. “Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi, sijawafuata Mabaali’? Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni; fikiri uliyoyafanya. Wewe ni ngamia jike mwenye mbio ukikimbia hapa na pale, punda-mwitu aliyezoea jangwa, anayenusa upepo katika tamaa yake kubwa: wakati wake wa kuhitaji mbegu ni nani awezaye kumzuia? Madume yoyote yanayomfuatilia hayana haja ya kujichosha; wakati wa kupandwa kwake yatampata tu. Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu, na koo lako liwe limekauka. Lakini ulisema, ‘Haina maana! Ninaipenda miungu ya kigeni, nami lazima niifuatie.’ “Kama vile mwizi anavyoaibika akikamatwa, hivyo ndivyo nyumba ya Israeli inavyoaibishwa: wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao. Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’ nalo jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’ Wamenipa visogo vyao wala hawakunigeuzia nyuso zao; lakini wakiwa katika taabu, wanasema, ‘Njoo utuokoe!’ Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea? Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa wakati mko katika taabu! Kwa maana mna miungu mingi kama mlivyo na miji, ee Yuda. “Kwa nini mnaleta mashtaka dhidi yangu? Ninyi nyote mmeniasi,” asema BWANA. “Nimeadhibu watu wako bure tu, hawakujirekebisha. Upanga wako umewala manabii wako kama simba mwenye njaa.