Isaya 7:21-25
Isaya 7:21-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, mtu atafuga ng'ombe mmoja mchanga na kondoo wawili; nao watatoa maziwa kwa wingi hata aweze kula siagi. Watu watakaosalia katika nchi watakula siagi na asali. Wakati huo, kila mahali palipokuwa na mashamba ya mizabibu kwa maelfu ya thamani ya fedha 1,000 kwa kipimo cha hekalu yatakuwa mbigili na miiba mitupu. Watu watakwenda huko kuwinda kwa pinde na mishale, maana nchi yote itakuwa imejaa mbigili na miiba. Nayo milima yote iliyokuwa ikilimwa itakuwa imejaa mbigili na miiba, hata hakuna mtu atakayejaribu kwenda huko, badala yake itakuwa malisho ya ng'ombe na kondoo.
Isaya 7:21-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika siku hiyo itakuwa ya kwamba mtu atalisha ng'ombe jike mchanga na kondoo wawili wa kike; kisha itakuwa, kwa sababu wanyama hao watatoa maziwa mengi, atakula siagi; kwa maana kila mtu aliyesalia katika nchi hii atakula siagi na asali. Tena itakuwa katika siku hiyo kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja, iliyopata fedha elfu moja, patakuwa mahali pa mbigili na miiba tu. Mtu atakayekwenda huko atakwenda na mishale na upinde; kwa sababu nchi yote itakuwa ina mbigili na miiba. Na vilima vyote vilivyolimwa kwa jembe, hutafika huko kwa sababu ya kuiogopa mbigili na miiba, lakini hapo patakuwa mahali pa kupeleka ng'ombe, mahali pa kukanyagwa na kondoo.
Isaya 7:21-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika siku hiyo itakuwa ya kwamba mtu atalisha ng’ombe mke mchanga na kondoo wake wawili; kisha itakuwa, kwa sababu wanyama hao watatoa maziwa mengi, atakula siagi; kwa maana kila mtu aliyesalia katika nchi hii atakula siagi na asali. Tena itakuwa katika siku hiyo kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu, iliyopata fedha elfu, patakuwa mahali pa mbigili na miiba tu. Mtu atakayekwenda huko atakwenda na mishale na upinde; kwa sababu nchi yote itakuwa ina mibigili na miiba. Na vilima vyote vilivyolimwa kwa jembe, hutafika huko kwa sababu ya kuiogopa mibigili na miiba, lakini hapo patakuwa mahali pa kupeleka ng’ombe, mahali pa kukanyagwa na kondoo.
Isaya 7:21-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika siku ile, mtu atahifadhi hai mtamba mmoja na kondoo wawili. Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali. Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli elfu moja za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu. Watu wataenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba. Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtaenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba. Patakuwa mahali ngʼombe wataachiwa huru, na kondoo kukimbia kimbia.