Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 7

7
Ujumbe kwa mfalme Ahazi
1 #7:1 Taz 2Fal 16:5; 2Nya 28:5-6 Wakati mfalme Ahazi mwana wa Yothamu na mjukuu wa Uzia, alipokuwa anatawala Yuda, Resini, mfalme wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, waliushambulia mji wa Yerusalemu, lakini hawakuweza kuuteka. 2Mfalme wa Yuda alipopata habari kwamba Waashuru wanashirikiana na Waisraeli, yeye pamoja na watu wote wa Yuda waliogopa na kutetemeka kama miti inayotikiswa na upepo.
3Mwenyezi-Mungu akamwambia Isaya, “Mchukue mwanao, Shearyashubu,#7:3 Shearyashubu: Maana yake watakaobaki watarudi. uende kukutana na mfalme Ahazi. Utamkuta barabarani mahali wanapofanyia kazi watengenezaji nguo, mwisho wa mfereji uletao maji kutoka bwawa la juu. 4Mwambie awe macho, atulie na asiogope wala asife moyo, kwa sababu ya hasira kali ya mfalme Resini wa Ashuru, na ya mwana wa Remalia. Hao wawili ni kama tu moshi wa kuni zinazozimika. 5Waashuru, kadhalika na Peka pamoja na jeshi la Efraimu wamefanya mpango mbaya dhidi yako. Wamesema, 6‘Twende kuivamia nchi ya Yuda, tuwatie watu hofu, tuitwae nchi na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme wao.’
7“Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Jambo hilo halitafaulu kamwe.
8,9Kwani mji mkuu wa Aramu ni Damasko,
na huyo Resini ni mkuu wa Damasko tu.
Mji mkuu wa Efraimu ni Samaria,
na mwana wa Remalia ni mkuu wa Samaria tu.
Mnamo miaka sitini na mitano utawala wa Efraimu utavunjwa;
Efraimu halitakuwa taifa tena.
Kama hutaamini hutaimarika.”
Ishara ya Emanueli
10Tena Mwenyezi-Mungu akamwambia Ahazi, 11“Mwombe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, akupe ishara; iwe ni kutoka chini kuzimu au juu mbinguni.” 12Ahazi akajibu, “Sitaomba ishara! Sitaki kumjaribu Mwenyezi-Mungu.” 13Basi, Isaya akamjibu, “Sikiliza basi, enyi watu wa ukoo wa Daudi! Je, haitoshi kuwachosha watu hata sasa mnataka kumchosha Mungu wangu pia? 14#7:14 Taz Mat 1:23 Haya basi, Bwana mwenyewe atawapa ishara: Msichana atachukua mimba, atajifungua mtoto wa kiume na kumwita jina lake Emanueli.#7:14 Emanueli: Maana yake Mungu yu pamoja nasi. 15Atakula siagi na asali mpaka atakapojua kukataa mabaya na kuchagua mema. 16Maana, kabla mtoto huyo hajajua kukataa maovu na kuchagua mema, nchi za wafalme hao wawili unaowaogopa zitakuwa mahame. 17Mwenyezi-Mungu atakuletea wewe pamoja na watu wako na jamii yote ya kifalme siku za taabu kuliko zile zote zilizowahi kutokea tangu wakati watu wa Efraimu walipojitenga na Yuda; yaani, atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”
18Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atawapigia mruzi watu wa Misri waje kama nzi toka vijito vya mto Nili; na watu wa Ashuru waje kama nyuki kutoka nchi yao. 19Watakuja makundi kwa makundi na kuyajaza mabonde yaliyopasukapasuka, mapango miambani, miiba, vichaka vyote na malisho yote.
20Wakati huo, Bwana atakopa wembe kutoka ngambo ya mto Eufrate, yaani mfalme wa Ashuru. Atawanyoa vichwa vyenu, miili yenu na kukatilia mbali pia ndevu zenu.
21Wakati huo, mtu atafuga ng'ombe mmoja mchanga na kondoo wawili; 22nao watatoa maziwa kwa wingi hata aweze kula siagi. Watu watakaosalia katika nchi watakula siagi na asali.
23Wakati huo, kila mahali palipokuwa na mashamba ya mizabibu kwa maelfu ya thamani ya fedha 1,000 kwa kipimo cha hekalu yatakuwa mbigili na miiba mitupu. 24Watu watakwenda huko kuwinda kwa pinde na mishale, maana nchi yote itakuwa imejaa mbigili na miiba. 25Nayo milima yote iliyokuwa ikilimwa itakuwa imejaa mbigili na miiba, hata hakuna mtu atakayejaribu kwenda huko, badala yake itakuwa malisho ya ng'ombe na kondoo.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 7: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha