Isaya 56:1-8
Isaya 56:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema: “Zingatieni haki na kutenda mema, maana nitawaokoeni hivi karibuni, watu wataona wazi kwamba ninawakomboeni. Heri mtu anayezingatia kikamilifu ninayosema, anayeshika sheria ya Sabato kwa heshima na kuepa kutenda uovu wowote. “Mgeni anayenitambua mimi Mwenyezi-Mungu asifikiri: ‘Hakika Mwenyezi-Mungu atanitenga na watu wake.’ Naye towashi asiseme: ‘Mimi ni mti mkavu tu!’ Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Towashi ashikaye sheria zangu za Sabato, anayefanya mambo yanayonipendeza, na kulizingatia agano langu, nitampa nafasi maalumu na ya sifa katika nyumba yangu na kuta zake; nafasi bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike: Nitampa jina la kukumbukwa daima, na ambalo halitafutwa kamwe. “Watu wageni watakaonikiri mimi Mwenyezi-Mungu, watakaoniheshimu, wakapenda jina langu na kuwa watumishi wangu, wote watakaoshika Sabato bila kuikufuru, watu watakaozingatia agano langu, hao nitawaleta katika mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; tambiko na sadaka zao zitakubaliwa madhabahuni pangu. Maana nyumba yangu itaitwa: ‘Nyumba ya sala kwa ajili ya watu wote’. “Hii ni kauli yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu ninayewakusanya Waisraeli waliotawanyika. Licha ya hao niliokwisha kukusanya, nitawakusanya watu wengine wajumuike nao.”
Isaya 56:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu uko karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote. Wala mgeni, aambatanaye na BWANA, asiseme hivi, Hakika yake BWANA atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu. Kwa maana BWANA awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu; Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali. Na wageni, walioandamana na BWANA ili wamhudumu, na kulipenda jina la BWANA, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hadi katika mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.
Isaya 56:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wo wote. Wala mgeni, aambatanaye na BWANA, asiseme hivi, Hakika yake BWANA atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu. Kwa maana BWANA awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu; Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali. Na wageni, walioandamana na BWANA ili wamhudumu, na kulipenda jina la BWANA, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.
Isaya 56:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo asemalo BWANA: “Dumisheni haki na mkatende lile lililo sawa, kwa maana wokovu wangu u karibu na haki yangu itafunuliwa upesi. Amebarikiwa mtu yule atendaye hili, mtu yule alishikaye kwa uthabiti, yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.” Usimwache mgeni aambatanaye na BWANA aseme, “Hakika BWANA atanitenga na watu wake.” Usimwache towashi yeyote alalamike akisema, “Mimi ni mti mkavu tu.” Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa matowashi washikao Sabato zangu, ambao huchagua kile kinachonipendeza na kulishika sana agano langu: hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake kumbukumbu na jina bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike: nitawapa jina lidumulo milele, ambalo halitakatiliwa mbali. Wageni wanaoambatana na BWANA ili kumtumikia, kulipenda jina la BWANA, na kumwabudu yeye, wote washikao Sabato bila kuinajisi na ambao hushika sana agano langu: hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala. Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao zitakubalika juu ya madhabahu yangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.” BWANA Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye Waisraeli waliohamishwa: “Bado nitawakusanya wengine kwao zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.”