Isaya 43:14-19
Isaya 43:14-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi: “Kwa ajili yenu nitatuma jeshi Babuloni. Nitayavunjilia mbali malango ya mji wake, na kelele za hao Wakaldayo zitageuka maombolezo. Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wenu; Mimi ndimi Muumba wa Israeli, Mfalme wenu.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wakati mmoja nilifanya barabara baharini nikaweka njia kati ya mawimbi makubwa. Nililipiga jeshi lenye nguvu, jeshi la magari na farasi wa vita, askari na mashujaa wa vita. Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena, niliwakomesha na kuwazima kama utambi wa taa. Sasa nasema: ‘Msiyanganganie mambo yaliyopita, wala msifikirie vitu vya zamani. Tazameni, mimi ninafanya kitu kipya. Kinafanyika sasa hivi, nanyi mtaweza kukiona. Nitafanya njia nyikani, na kububujisha mito jangwani.
Isaya 43:14-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia. Mimi ni BWANA, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu. BWANA asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa kama utambi. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.
Isaya 43:14-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia. Mimi ni BWANA, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu. BWANA asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.
Isaya 43:14-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo asemalo BWANA, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa ajili yenu nitatumana Babeli na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi, katika meli walizozionea fahari. Mimi ndimi BWANA, yeye Aliye Mtakatifu wako, Muumba wa Israeli, Mfalme wako.” Hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyefanya njia baharini, mahali pa kupita kwenye maji mengi, aliyeyakokota magari ya vita na farasi, jeshi pamoja na askari wa msaada, nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe, wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi: “Msiyakumbuke mambo yaliyopita, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitafanya jambo jipya! Sasa litachipuka, je, hamtalitambua? Nitafanya njia jangwani na vijito vya maji katika nchi kame.