Isaya 43:1-7
Isaya 43:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu aliyewaumba enyi watu wa Yakobo, yeye aliyewafanya enyi watu wa Israeli, asema: “Msiogope, maana mimi nimewakomboa; nimewaita kwa jina nanyi ni wangu. Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza. Maana mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Mungu Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wenu. Nitaitoa nchi ya Misri iwe fidia yenu, nitaitoa Kushi na Seba ili mwachwe huru. Kwa vile mna thamani mbele yangu, kwa kuwa nimewapa hadhi na kuwapenda, mimi nawaacha watu kusudi niwapate nyinyi, nayaachilia mataifa badala ya maisha yenu. Msiogope maana mimi nipo pamoja nanyi. “Nitawarudisha wazawa wenu toka mashariki, nitawakusanyeni kutoka magharibi. Nitaiambia kaskazini, ‘Waache waondoke’, na kusini, ‘Usiwazuie’! Warudisheni watu kutoka mbali, kutoka kila mahali duniani. Kila mmoja hujulikana kwa jina langu, niliwaumba wote na kuwafanya kwa ajili ya utukufu wangu.”
Isaya 43:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na makabila ya watu kwa ajili ya maisha yako. Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.
Isaya 43:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako. Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.
Isaya 43:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini sasa hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyekuumba, ee Yakobo, yeye aliyekuhuluku, ee Israeli: “Usiogope kwa maana nimekukomboa, nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu. Unapopita kwenye maji makuu, nitakuwa pamoja nawe, unapopita katika mito ya maji, hayatakugharikisha. Utakapopita katika moto, hutaungua, miali ya moto haitakuunguza. Kwa kuwa Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako. Ninaitoa Misri kuwa fidia yako, Kushi na Seba badala yako. Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu, nami kwa kuwa ninakupenda, nitatoa watu badala yako na mataifa badala ya maisha yako. Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe, nitawaleta watoto wako kutoka mashariki, na kukukusanya kutoka magharibi. Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’ nayo kusini, ‘Usiwazuie.’ Walete wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia: kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu, niliyemuumba kwa utukufu wangu, niliyemhuluku na kumfanya.”