Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 31:1-9

Isaya 31:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

Ole wao wale waendao Misri kuomba msaada, ole wao wanaotegemea farasi, wanaotegemea wingi wa magari yao ya vita, na nguvu za askari wao wapandafarasi, nao hawamtegemei Mtakatifu wa Israeli, wala hawamwombi Mwenyezi-Mungu shauri! Mungu ni mwenye busara na huleta maangamizi. Habadilishi tamko lake; ila yuko tayari kuwakabili watu waovu kadhalika na wasaidizi wa watendao mabaya. Wamisri ni binadamu tu wala si Mungu; farasi wao nao ni wanyama tu, si roho. Mwenyezi-Mungu akiunyosha mkono wake, taifa linalotoa msaada litajikwaa, na lile linalosaidiwa litaanguka; yote mawili yataangamia pamoja. Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Kama vile simba au mwanasimba angurumavyo kuyakinga mawindo yake, hata kundi la wachungaji likiitwa kumkabili, yeye hatishiki kwa kelele zao, wala hashtuki kwa sauti zao. Ndivyo atakavyoshuka Mwenyezi-Mungu wa majeshi kupigana juu ya mlima Siyoni na kilima chake. Kama ndege arukavyo juu ya viota vyake, ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyoulinda Yerusalemu, ataulinda na kuukomboa, atauhifadhi na kuuokoa. Enyi Waisraeli, mrudieni huyo mliyemsaliti vibaya. Wakati utafika ambapo nyote mtavitupilia mbali vinyago vyenu vya fedha na dhahabu ambavyo mmejitengenezea kwa mikono yenu, vikawakosesha. Hapo Waashuru watauawa kwa upanga, lakini si kwa upanga wa binadamu; naam, wataangamizwa kwa upanga ambao ni zaidi ya ule wa binadamu. Waashuru watakimbia na vijana wao watafanyizwa kazi za kitumwa. Mfalme wao atatoroka kwa hofu, na maofisa wao wataiacha bendera yao kwa woga. Hayo ameyatamka Mwenyezi-Mungu ambaye moto wake umo mjini Siyoni, naam, tanuri lake limo mjini Yerusalemu.”

Shirikisha
Soma Isaya 31

Isaya 31:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ole wao wateremkao kwenda Misri wapate msaada, na kutegemea farasi; watumainio magari kwa kuwa ni mengi, na wapanda farasi kwa kuwa ni hodari sana; lakini hawamwangalii Mtakatifu wa Israeli, wala hawamtafuti BWANA! Lakini yeye naye ana akili, naye ataleta uovu, wala hatayatangua maneno yake; bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada wa hao watendao maovu. Basi Wamisri ni wanadamu wala si Mungu, na farasi wao ni nyama wala si roho; na BWANA atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wataangamia wote pamoja. Maana BWANA aniambia hivi, Kama vile ilivyo simba angurumapo na mwanasimba juu ya mawindo yake, wachungaji wengi wakiitwa ili kumpiga, lakini hatiwi hofu na sauti zao, wala kufanya woga kwa sababu ya mshindo wao; ndivyo BWANA wa majeshi atakavyoshuka ili kufanya vita juu ya mlima Sayuni, na juu ya kilima chake. Kama ndege warukao, BWANA wa majeshi ataulinda Yerusalemu; ataulinda na kuuokoa, atapita juu yake na kuuhifadhi. Mwelekeeni yeye mliyemwasi sana, enyi wana wa Israeli. Maana katika siku hiyo kila mtu atatupa sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, ambazo mikono yenu imezifanya, zikawa dhambi kwenu. Ndipo huyo Mwashuri ataanguka kwa upanga ambao si wa mtu; na upanga usio upanga wa mtu utamwangamiza; naye ataukimbia upanga, na vijana wake watatoa kodi. Na mwamba wake utatoweka kwa sababu ya hofu, nao wakuu wake wataionea bendera hofu kuu, asema BWANA, ambaye moto wake u katika Sayuni, na tanuri yake katika Yerusalemu.

Shirikisha
Soma Isaya 31

Isaya 31:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ole wao watelemkao kwenda Misri wapate msaada, na kutegemea farasi; watumainio magari kwa kuwa ni mengi, na wapanda farasi kwa kuwa ni hodari sana; lakini hawamwangalii Mtakatifu wa Israeli, wala hawamtafuti BWANA! Lakini yeye naye ana akili, naye ataleta uovu, wala hatayatangua maneno yake; bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada wa hao watendao maovu. Basi Wamisri ni wanadamu wala si Mungu, na farasi zao ni nyama wala si roho; na BWANA atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wote pamoja watakoma. Maana BWANA aniambia hivi, Kama vile ilivyo simba angurumapo na mwana-simba juu ya mawindo yake, wachungaji wengi wakiitwa ili kumpiga, lakini hatiwi hofu na sauti zao, wala kufanya woga kwa sababu ya mshindo wao; ndivyo BWANA wa majeshi atakavyoshuka ili kufanya vita juu ya mlima Sayuni, na juu ya kilima chake. Kama ndege warukao, BWANA wa majeshi ataulinda Yerusalemu; ataulinda na kuuokoa, atapita juu yake na kuuhifadhi. Mwelekeeni yeye mliyemwasi sana, enyi wana wa Israeli. Maana katika siku hiyo kila mtu atatupa sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, ambazo mikono yenu imezifanya, zikawa dhambi kwenu. Ndipo huyo Mwashuri ataanguka kwa upanga ambao si wa mtu; na upanga usio upanga wa mtu utamla; naye ataukimbia upanga, na vijana wake watatoa kodi. Na mwamba wake utatoweka kwa sababu ya hofu, nao wakuu wake wataionea bendera hofu kuu, asema BWANA, ambaye moto wake u katika Sayuni, na tanuru yake katika Yerusalemu.

Shirikisha
Soma Isaya 31

Isaya 31:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ole wao wale wanaoshuka Misri kutafuta msaada, wale wanaotegemea farasi, wanaoweka tumaini katika wingi wa magari yao ya vita, na katika nguvu nyingi za wapanda farasi, lakini hawamwangalii yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, wala hawatafuti msaada kwa BWANA. Hata hivyo yeye pia ana hekima na anaweza kuleta maafa, wala hayatangui maneno yake. Yeye atainuka dhidi ya nyumba ya mwovu, dhidi ya wale ambao huwasaidia watenda maovu. Lakini Wamisri ni wanadamu, wala si Mungu, farasi wao ni nyama, wala si roho. BWANA atakaponyoosha Mkono wake, yeye anayesaidia atajikwaa, naye anayesaidiwa ataanguka, wote wawili wataangamia pamoja. Hili ndilo BWANA analoniambia: “Kama vile simba angurumavyo, simba mkubwa juu ya mawindo yake: hata ingawa kundi lote la wafugaji huitwa pamoja dhidi yake, hatiwi hofu na kelele zao, wala kusumbuliwa na ghasia zao; ndivyo BWANA wa majeshi atakavyoshuka kufanya vita juu ya Mlima Sayuni na juu ya vilele vyake. Kama ndege warukao, BWANA wa majeshi ataukinga Yerusalemu; ataukinga na kuuokoa, atapita juu yake na kuufanya salama.” Mrudieni yeye ambaye nyumba ya Israeli imemwasi sana. Kwa kuwa katika siku ile kila mmoja wenu atazikataa sanamu za fedha na za dhahabu zilizotengenezwa kwa mikono yenu yenye dhambi. “Ashuru itaanguka kwa upanga ambao si wa mwanadamu; upanga usio wa kibinadamu utawaangamiza. Watakimbia mbele ya upanga na vijana wao wa kiume watafanyizwa kazi kwa lazima. Ngome zao zitaanguka kwa sababu ya hofu; kwa kuona bendera ya vita, majemadari wao watashikwa na hofu ya ghafula,” asema BWANA, ambaye moto wake uko Sayuni, nalo tanuru lake liko Yerusalemu.

Shirikisha
Soma Isaya 31