Isaya 30:18-26
Isaya 30:18-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu anangoja awafadhili, atainuka na kuwaonea huruma. Maana, Mwenyezi-Mungu ni Mungu atendaye haki. Heri wote wale wanaomtumainia. Enyi watu wa Siyoni, enyi watu wa Yerusalemu, hakika nyinyi hamtaomboleza tena. Kweli Mungu atawahurumia; mara tu atakaposikia kilio chenu atawaitikeni. Ingawa Bwana atawalisha taabu na kuwanywesha dhiki, yeye ndiye Mwalimu wenu na hatajificha tena; nanyi mtamwona kwa macho yenu wenyewe. Mkienda kulia au kushoto, mtasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Njia ni hii; ifuateni.” Mtavifanya haramu vinyago vyenu vya miungu vilivyopakwa fedha na sanamu zenu zilizopakwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitu najisi, mkisema, “Poteleeni mbali!” Mtakapopanda mbegu zenu, Mwenyezi-Mungu atanyesha mvua kwa wakati wake, nazo zitakua na kuwapa mavuno mengi. Mifugo yenu nayo itapata malisho kwa wingi. Mafahali na punda wenu wa kulimia watapata malisho yaliyochambuliwa vizuri na kutiwa chumvi. Wakati utakapofika ambapo maadui watauawa na ngome zao kubomolewa, vijito vya maji vitatiririka kutoka kila mlima na kilima. Tena mwezi utawaka kama jua, nao mwanga wa jua utakuwa mara saba ya mwanga wake wa kawaida, kana kwamba mwanga wa siku saba umeangaza katika siku moja. Mambo haya yote yatatukia wakati Mwenyezi-Mungu atakapoyafunga na kuyaponya majeraha aliyowaletea watu wake.
Isaya 30:18-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao. Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng'ombe wako watakula katika malisho mapana. Ng'ombe pia na wanapunda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha lao.
Isaya 30:18-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao. Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.
Isaya 30:18-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hata hivyo BWANA anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonyesha huruma. Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye! Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!” Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ngʼombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana. Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utangʼaa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati BWANA atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia.