Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 30:18-26

Isaya 30:18-26 NEN

Hata hivyo BWANA anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonyesha huruma. Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye! Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!” Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ngʼombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana. Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utangʼaa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati BWANA atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha