Isaya 29:1-16
Isaya 29:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wako Yerusalemu, madhabahu ya Mungu; mji ambamo Daudi alipiga kambi yake! Miaka yaja na kupita, na sikukuu zako zaendelea kufanyika; lakini mimi Mungu nitauhuzunisha Yerusalemu, nako kutakuwa na vilio na maombolezo, mji wenyewe utakuwa kama madhabahu iliyolowa damu ya watu waliouawa. Mimi nitapanga jeshi dhidi ya Yerusalemu, nami nitauzingira na kuushambulia. Utaangushwa mbali sana ndani ya ardhi; kutoka huko mbali utatoa sauti; maneno yako yatatoka huko chini mavumbini; sauti yako itatoka ardhini kama ya mzimu. Kundi la maadui zako litakuwa kama vumbi laini, waliokutendea ukatili watakuwa kama makapi. Hayo yatafanyika ghafla. Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuja kukusaidia; atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi na sauti kubwa; atakuja na kimbunga, tufani na moto uunguzao. Hapo, kundi la mataifa yote yanayoshambulia Yerusalemu, wote wanaoshambulia ngome yake na kuutia wasiwasi, watatoweka kama ndoto, kama maono ya usiku. Mataifa yote yanayoushambulia mji wa Yerusalemu yatakuwa kama mtu mwenye njaa anayeota anakula lakini aamkapo bado anaumwa na njaa! Au mtu mwenye kiu anayeota kuwa anakunywa, lakini anaamka mdhaifu, bado ana kiu. Endeleeni kuwa wapumbavu na kuduwaa! Jipofusheni na kuwa vipofu! Leweni lakini si kwa divai; pepesukeni lakini si kwa pombe. Mwenyezi-Mungu amewamiminia hali ya usingizi mzito; ameyafumba macho yenu enyi manabii, amefunika vichwa vyenu enyi waonaji. Basi, kwenu nyinyi maono yote haya ni kama ujumbe ulioandikwa katika kitabu kilichofungwa kwa mhuri. Ukimpelekea mtu yeyote ajuaye kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atasema, “Siwezi kukisoma kwani kimefungwa kwa mhuri.” Na ukimpa mtu yeyote asiyejua kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atakuambia, “Sijui kusoma.” Bwana asema, “Watu hawa huja kuniabudu kwa maneno matupu, hali mioyo yao iko mbali nami. Wananiheshimu kulingana na mapokeo ya watu tu, jambo walilojifunza wao wenyewe. Hivyo, nitawatenda tena watu hawa maajabu, mambo ya ajabu na ya kushangaza. Nao wenye hekima wao wataishiwa hekima, na busara ya wenye busara wao itatoweka. “Ole mnaomficha Mwenyezi-Mungu mipango yenu, mnaotenda matendo yenu gizani na kusema: ‘Hamna atakayetuona; nani awezaye kujua tunachofanya?’ Nyinyi mnafanya mambo kinyume kabisa! Je, mfinyanzi na udongo ni hali moja? Chombo hakiwezi kumwambia aliyekitengeneza: ‘Wewe hukunitengeneza.’ Kilichofinyangwa hakiwezi kumwambia aliyekiumba, ‘Wewe hujui chochote.’”
Isaya 29:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wa Arieli, Arieli, mji ambao Daudi alifanya kituo chake ndani yake; ongezeni mwaka baada ya mwaka; sikukuu na zirudi wakati wake, ndipo nitamwudhi Arieli; kutakuwapo maombolezo na kilio; naye atakuwa kwangu kama Arieli. Nami nitapiga kimo juu yako pande zote, nitakuhusuru kwa ngome, nami nitajenga maboma yakuzunguke. Nawe utashushwa, nawe utanena toka chini ya nchi, na maneno yako yatakuwa chini toka mavumbini; na sauti yako itakuwa kama sauti ya mtu mwenye pepo, ikitoka katika nchi, na matamko yako yatanong'ona toka mavumbini. Lakini wingi wa adui zako utakuwa kama mavumbi laini, na wingi wao watishao utakuwa kama makapi yapitayo; naam, itakuwa mara na kwa ghafla. Naye atajiliwa na BWANA wa majeshi kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sauti kuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao. Na wingi wa mataifa wapiganao na Arieli, wote wapiganao naye na ngome yake, na wanaomwudhi, watakuwa kama ndoto, na maono ya usiku. Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani; hivyo ndivyo utakavyokuwa huo wingi wa mataifa waletao vita juu ya mlima Sayuni. Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewayawaya wala si kwa sababu ya kileo. Kwa maana BWANA amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji. Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya kitabu kilichotiwa mhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa mhuri; kisha kitabu hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi. Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walichonacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa; kwa sababu hiyo mimi nitafanya tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa. Ole wao wanaojitahidi kumficha BWANA mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye? Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?
Isaya 29:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wa Arieli, Arieli, mji ambao Daudi alifanya kituo chake ndani yake; ongezeni mwaka baada ya mwaka; sikukuu na zirudi wakati wake, ndipo nitamwudhi Arieli; kutakuwapo maombolezo na kilio; naye atakuwa kwangu kama Arieli. Nami nitapiga kimo juu yako pande zote, nitakuhusuru kwa ngome, nami nitajenga maboma yakuzunguke. Nawe utashushwa, nawe utanena toka chini ya nchi, na maneno yako yatakuwa chini toka mavumbini; na sauti yako itakuwa kama sauti ya mtu mwenye pepo, ikitoka katika nchi, na matamko yako yatanong’ona toka mavumbini. Lakini wingi wa adui zako utakuwa kama mavumbi membamba, na wingi wao watishao utakuwa kama makapi yapitayo; naam, itakuwa mara na kwa ghafula. Naye atajiliwa na BWANA wa majeshi kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sauti kuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao. Na wingi wa mataifa wapiganao na Arieli, wote wapiganao naye na ngome yake, nao wamwudhio, watakuwa kama ndoto, na maono ya usiku. Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani; hivyo ndivyo utakavyokuwa huo wingi wa mataifa waletao vita juu ya mlima Sayuni. Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewaya-waya wala si kwa sababu ya kileo. Kwa maana BWANA amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji. Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri; kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi. Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa; kwa sababu hiyo mimi nitafanya tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa. Ole wao wanaojitahidi kumficha BWANA mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye? Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?
Isaya 29:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ole wako, wewe Arieli, Arieli, mji alimokaa Daudi! Ongezeni mwaka kwa mwaka, na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee. Hata hivyo nitauzingira Arieli kwa jeshi, utalia na kuomboleza, utakuwa kwangu kama mahali pa kuwashia moto madhabahuni. Nitapiga kambi pande zote dhidi yako, nitakuzunguka kwa minara na kujenga ngome yakukuzingira. Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini, utamumunya maneno yako kutoka mavumbini. Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu, utanongʼona maneno yako toka mavumbini. Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini; makundi ya watu wakatili watakuwa kama makapi yanayopeperushwa. Naam, ghafula, mara moja, BWANA wa majeshi atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu, atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo. Kisha makundi ya mataifa yote yanayopigana dhidi ya Arieli, yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzingira kwa jeshi, watakuwa kama ilivyo ndoto, kama maono wakati wa usiku: kama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula, lakini huamka, bado njaa yake ingalipo, kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji, lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu. Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni. Pigweni na butwaa na mshangae; jifanyeni vipofu wenyewe na msione; leweni, lakini si kwa mvinyo, pepesukeni lakini si kwa kileo. BWANA amewaleteeni usingizi mzito: Ameziba macho yenu ninyi manabii; amefunika vichwa vyenu ninyi waonaji. Kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa muhuri katika kitabu. Mkimpa mtu yeyote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri.” Au mkimpa mtu yeyote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.” Bwana asema: “Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao na kuniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Ibada yao kwangu inatokana na maagizo waliyofundishwa na wanadamu. Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa, kwa ajabu juu ya ajabu. Hekima ya wenye hekima itapotea, nayo akili ya wenye akili itatoweka.” Ole kwa wale wanaoenda kwenye vilindi virefu kumficha BWANA mipango yao, wafanyao kazi zao gizani na kufikiri, “Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?” Mnapindua mambo juu chini, kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi! Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga, “Wewe hukunifinyanga mimi”? Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi, “Wewe hujui chochote”?