Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 29

29
Ujumbe dhidi ya Yerusalemu
1Ole wako Yerusalemu, madhabahu ya Mungu;#29:1 madhabahu ya Mungu; ni tafsiri ya neno la Kiebrania Arieli ambalo katika Ezekieli 43:15,16 linamaanisha sehemu ya juu ya madhabahu. Arieli hapa ni jina la kishairi la Yerusalemu!
mji ambamo Daudi alipiga kambi yake!
Miaka yaja na kupita,
na sikukuu zako zaendelea kufanyika;
2lakini mimi Mungu nitauhuzunisha Yerusalemu,
nako kutakuwa na vilio na maombolezo,
mji wenyewe utakuwa kama madhabahu
iliyolowa damu ya watu waliouawa.
3Mimi nitapanga jeshi dhidi ya Yerusalemu,
nami nitauzingira na kuushambulia.
4Utaangushwa mbali sana ndani ya ardhi;
kutoka huko mbali utatoa sauti;
maneno yako yatatoka huko chini mavumbini;
sauti yako itatoka ardhini kama ya mzimu.
5Kundi la maadui zako litakuwa kama vumbi laini,
waliokutendea ukatili watakuwa kama makapi.
Hayo yatafanyika ghafla.
6Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuja kukusaidia;
atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi na sauti kubwa;
atakuja na kimbunga, tufani na moto uunguzao.
7Hapo, kundi la mataifa yote yanayoshambulia Yerusalemu,
wote wanaoshambulia ngome yake na kuutia wasiwasi,
watatoweka kama ndoto, kama maono ya usiku.
8Mataifa yote yanayoushambulia mji wa Yerusalemu
yatakuwa kama mtu mwenye njaa anayeota anakula
lakini aamkapo bado anaumwa na njaa!
Au mtu mwenye kiu anayeota kuwa anakunywa,
lakini anaamka mdhaifu, bado ana kiu.
Hatari ya kupuuza maonyo
9Endeleeni kuwa wapumbavu na kuduwaa!
Jipofusheni na kuwa vipofu!
Leweni lakini si kwa divai;
pepesukeni lakini si kwa pombe.
10 #29:10 Taz Rom 11:8 Mwenyezi-Mungu amewamiminia hali ya usingizi mzito;
ameyafumba macho yenu enyi manabii,
amefunika vichwa vyenu enyi waonaji.
11Basi, kwenu nyinyi maono yote haya ni kama ujumbe ulioandikwa katika kitabu kilichofungwa kwa mhuri. Ukimpelekea mtu yeyote ajuaye kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atasema, “Siwezi kukisoma kwani kimefungwa kwa mhuri.” 12Na ukimpa mtu yeyote asiyejua kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atakuambia, “Sijui kusoma.”
13 #29:13 Taz Mat 15:8-9 Marko 7:6-7 Bwana asema,
“Watu hawa huja kuniabudu kwa maneno matupu,
hali mioyo yao iko mbali nami.
Wananiheshimu kulingana na mapokeo ya watu tu,
jambo walilojifunza wao wenyewe.
14 #29:14 Taz 1Kor 1:19 Hivyo, nitawatenda tena watu hawa maajabu,
mambo ya ajabu na ya kushangaza.
Nao wenye hekima wao wataishiwa hekima,
na busara ya wenye busara wao itatoweka.
Tumaini siku za usoni
15“Ole mnaomficha Mwenyezi-Mungu mipango yenu,
mnaotenda matendo yenu gizani
na kusema: ‘Hamna atakayetuona;
nani awezaye kujua tunachofanya?’
16 #29:16 Taz Isa 45:9; Rom 9:20 Nyinyi mnafanya mambo kinyume kabisa!
Je, mfinyanzi na udongo ni hali moja?
Chombo hakiwezi kumwambia aliyekitengeneza:
‘Wewe hukunitengeneza.’
Kilichofinyangwa hakiwezi kumwambia aliyekiumba,
‘Wewe hujui chochote.’”
Marekebisho makubwa
17Bado kidogo tu,
msitu wa Lebanoni utageuzwa kuwa shamba lenye rutuba,
na shamba lenye rutuba kuwa msitu.
18Siku hiyo viziwi watasikia ujumbe ukisomwa kitabuni
na kutoka gizani vipofu wataanza kuona.
19Wanyofu watapata furaha mpya kwa Mwenyezi-Mungu,
na maskini wa watu watashangilia kwa furaha
kwa sababu ya Mungu, Mtakatifu wa Israeli.
20Majitu makatili yataangamizwa,
wenye kumdhihaki Mungu watakwisha,
wote wanaootea kutenda maovu watatokomezwa.
21Watatoweka wale wanaopotosha kesi ya mtu mahakamani,
watu wanaowafanyia hila mahakimu
na wasemao uongo kuwanyima haki yao wasio na hatia.
22Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu aliyemkomboa Abrahamu,
asema hivi kuhusu wazawa wa Yakobo:
“Wazawa wa Yakobo hawataaibishwa tena,
hawatainamisha vichwa vyao tena kwa aibu.
23Watakapowaona watoto wao,
watoto niliowajalia mimi mwenyewe,
watalitukuza jina langu mimi Mtakatifu wa Yakobo;
watakuwa na uchaji kwangu mimi Mungu wa Israeli.
24Waliopotoka rohoni watapata maarifa
na wenye kununa watakubali kufunzwa.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 29: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha