Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 1:1-14

Waebrania 1:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote. Yeye ni mngao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu. Mwana ni mkuu kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu kuliko jina lao. Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa Baba yako.” Wala hakusema juu ya malaika yeyote: “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu.” Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae, mzaliwa wa kwanza, ulimwenguni alisema: “Malaika wote wa Mungu na wamwabudu.” Lakini kuhusu malaika, alisema: “Amewafanya malaika wake kuwa upepo, na wahudumu wake ndimi za moto.” Lakini kuhusu Mwana, Mungu alisema: “Kiti chako cha enzi, ee Mungu, chadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki. Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako, amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa kuliko wenzako.” Na tena: “Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi. Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma.” Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.” Malaika ni nini ila roho wanaomtumikia Mungu na ambao hutumwa kuwasaidia wale watakaopokea wokovu?

Waebrania 1:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wa Mungu na chapa kamili ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi katika mkono wa kulia wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa maana ni kwa malaika yeyote yupi Mungu, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu. Na kuhusu malaika asema, Awafanya malaika wake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto. Lakini kuhusu Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya haki. Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio. Na tena, Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi, Na mbingu ni kazi za mikono yako; Hizo zitaharibika, bali wewe unadumu; Nazo zote zitachakaa kama nguo, Na kama mavazi utazikunjakunja, na kama mavazi zitabadilishwa; Lakini wewe u yeye yule, Na miaka yako haitakoma. Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wowote, Uketi mkono wa kulia Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?

Waebrania 1:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu. Na kwa habari za malaika asema, Afanyaye malaika wake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto. Lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio. Na tena, Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi, Na mbingu ni kazi za mikono yako; Hizo zitaharibika, bali wewe unadumu; Nazo zote zitachakaa kama nguo, Na kama mavazi utazizinga, nazo zitabadilika; Lakini wewe u yeye yule, Na miaka yako haitakoma. Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?

Waebrania 1:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu. Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni. Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao. Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wowote Mungu alipata kumwambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuzaa?” Au tena, “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu?” Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema, “Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.” Anenapo kuhusu malaika asema, “Huwafanya malaika wake kuwa pepo, watumishi wake kuwa miali ya moto.” Lakini kwa habari za Mwana asema, “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, kitadumu milele na milele, nayo haki itakuwa fimbo ya utawala ya ufalme wako. Umependa haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako kwa kukupaka mafuta ya furaha.” Pia asema, “Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu; zote zitachakaa kama vazi. Utazikungʼutakungʼuta kama joho, nazo zitachakaa kama vazi. Lakini wewe hubadiliki, nayo miaka yako haikomi kamwe.” Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wowote, “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako”? Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha