Mwanzo 31:1-20
Mwanzo 31:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, ikasikika kwamba watoto wa kiume wa Labani walinungunika na kusema, “Yakobo amenyakua kila kitu cha baba yetu; ndivyo alivyopata kuwa tajiri.” Yakobo alijua pia kuwa Labani hakumjali yeye kama hapo awali. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya wazee wako na kwa jamaa yako, nami nitakuwa pamoja nawe.” Basi Yakobo akataka Raheli na Lea waitwe; nao wakamwendea mbugani alikokuwa anachunga wanyama. Yakobo akawaambia, “Naona kuwa baba yenu hanijali tena kama hapo awali. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote. Hata hivyo yeye amenidanganya na kuubadilisha ujira wangu mara kumi. Lakini Mungu hakumruhusu kunidhuru. Kila mara baba yenu aliposema, ‘Wanyama wenye madoadoa ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi kundi lote lilizaa wanyama wenye madoadoa. Na kila aliposema, ‘Wanyama wenye milia ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi, kundi lote lilizaa wanyama wenye milia. Ndivyo Mungu alivyochukua wanyama wa baba yenu, akanipa mimi. “Wakati wa majira ya wanyama kupata mimba niliota ndoto, na katika ndoto hiyo niliona mabeberu wote waliopanda majike walikuwa wenye milia, madoadoa na mabakamabaka. Malaika wa Mungu akaongea nami katika ndoto hiyo, akaniita, ‘Yakobo,’ nami nikaitika, ‘Naam!’ Naye akaniambia, ‘Tazama mabeberu wote wanaowapanda majike wana milia, madoadoa na mabaka mabaka. Jambo hili limekuwa hivyo kwa sababu nimeona alivyokutendea Labani. Mimi ndimi yule Mungu aliyekutokea kule Betheli, mahali pale ulipoweka lile jiwe wakfu kwa kulimiminia mafuta na ambapo uliniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii urudi katika nchi yako.’” Raheli na Lea wakamjibu Yakobo, “Sisi hatuna tena sehemu au urithi wowote katika nyumba ya baba yetu! Aidha yeye anatuona sisi kama wageni, kwa maana ametuuza; na mali ileile tuliyonunuliwa nayo ndiyo anayotumia. Mali yote ambayo Mungu ameichukua kutoka kwa baba yetu ni yetu sisi na watoto wetu. Kwa hiyo, fanya hayo aliyokuagiza Mungu!” Basi, Yakobo akajitayarisha kusafiri, akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. Alichukua wanyama wake wote pamoja na mali yote aliyochuma huko Padan-aramu, akaanza safari ya kurudi nchini Kanaani kwa baba yake Isaka. Wakati huo Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya wanyama wake. Hivyo Raheli alipata nafasi ya kuiba vinyago vya miungu ya baba yake. Yakobo alimdanganya Labani, Mwaramu, kwa kuondoka bila kumjulisha.
Mwanzo 31:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote. Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama hapo awali. BWANA akamwambia Yakobo, Urudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe. Yakobo akatuma watu ili kuwaita Raheli na Lea waje malishoni kwenye mifugo wake. Akawaambia, Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama hapo awali. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwachia anidhuru. Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi. Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, niliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka. Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa. Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda kondoo wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutenda Labani. Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa. Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je, Imebakia sehemu au urithi kwa ajili yetu katika nyumba ya baba yetu? Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa? Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang'anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi, yoyote Mungu aliyokuambia, uyafanye. Ndipo Yakobo akaondoka, akapandisha wanawe na wakeze juu ya ngamia. Akachukua wanyama wake wote, na mali yake yote aliyokuwa amepata, na wanyama aliowapata katika Padan-aramu, ili afike kwa Isaka babaye katika nchi ya Kanaani. Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye. Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia.
Mwanzo 31:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote. Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi. BWANA akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe. Yakobo akatuma watu, akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia, Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru. Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. Hivi Mungu akamnyang’anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi. Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka. Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa. Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani. Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa. Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je! Imetubakia sehemu au urithi katika nyumba ya baba yetu? Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa? Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang’anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi yo yote Mungu aliyokuambia, uyafanye. Ndipo Yakobo akaondoka, akapandisha wanawe na wakeze juu ya ngamia. Akachukua wanyama wake wote, na mali yake yote aliyokuwa ameyapata, na wanyama aliowapata katika Padan-aramu, ili afike kwa Isaka babaye katika nchi ya Kanaani. Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye. Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia.
Mwanzo 31:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu, naye amepata utajiri huu wote kutokana na mali ya baba yetu.” Yakobo akatambua kwamba moyo wa Labani kwake umebadilika. Ndipo BWANA akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.” Hivyo Yakobo akatuma ujumbe kwa Raheli na Lea waje malishoni kwenye makundi yake. Akawaambia, “Naona moyo wa baba yenu kwangu umebadilika, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote, lakini baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru. Aliposema, ‘Wenye madoadoa watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye madoadoa. Aliposema, ‘Wenye mistari watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye mistari. Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi. “Majira ya kuzaliana niliota ndoto. Niliinua macho na kuona kwamba wale beberu waliokuwa wakiwapanda mbuzi walikuwa wana mistari, madoadoa na mabaka mabaka. Malaika wa Mungu akaniita katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’ Akaniambia, ‘Inua macho yako uone wale beberu wote wanaowapanda mbuzi wana mistari, madoadoa au mabaka mabaka, kwa maana nimeona yale yote Labani amekutendea. Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia nguzo mafuta, na ukaniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’ ” Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu? Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata mali tuliyolipiwa. Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.” Ndipo Yakobo akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. Naye akawaswaga wanyama wote mbele yake, pamoja na mali yote aliyokuwa amepata huko Padan-Aramu ili aende kwa baba yake Isaka katika nchi ya Kanaani. Labani alipokuwa ameenda kukata kondoo wake manyoya, Raheli aliiba miungu ya nyumbani mwa baba yake. Zaidi ya hayo, Yakobo alimdanganya Labani Mwaramu kwa kutokumwambia kwamba anakimbia.