Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 31:1-20

Mwanzo 31:1-20 NENO

Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu, naye amepata utajiri huu wote kutokana na mali ya baba yetu.” Yakobo akatambua kwamba moyo wa Labani kwake umebadilika. Ndipo BWANA akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.” Hivyo Yakobo akatuma ujumbe kwa Raheli na Lea waje malishoni kwenye makundi yake. Akawaambia, “Naona moyo wa baba yenu kwangu umebadilika, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote, lakini baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru. Aliposema, ‘Wenye madoadoa watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye madoadoa. Aliposema, ‘Wenye mistari watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye mistari. Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi. “Majira ya kuzaliana niliota ndoto. Niliinua macho na kuona kwamba wale beberu waliokuwa wakiwapanda mbuzi walikuwa wana mistari, madoadoa na mabaka mabaka. Malaika wa Mungu akaniita katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’ Akaniambia, ‘Inua macho yako uone wale beberu wote wanaowapanda mbuzi wana mistari, madoadoa au mabaka mabaka, kwa maana nimeona yale yote Labani amekutendea. Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia nguzo mafuta, na ukaniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’ ” Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu? Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata mali tuliyolipiwa. Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.” Ndipo Yakobo akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. Naye akawaswaga wanyama wote mbele yake, pamoja na mali yote aliyokuwa amepata huko Padan-Aramu ili aende kwa baba yake Isaka katika nchi ya Kanaani. Labani alipokuwa ameenda kukata kondoo wake manyoya, Raheli aliiba miungu ya nyumbani mwa baba yake. Zaidi ya hayo, Yakobo alimdanganya Labani Mwaramu kwa kutokumwambia kwamba anakimbia.