Mwanzo 27:14-20
Mwanzo 27:14-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yakobo akaenda, akachukua wanambuzi wawili, akamletea mama yake; naye akatayarisha chakula kitamu, kile apendacho Isaka baba yake. Kisha Rebeka akatwaa mavazi bora ya Esau, mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo, mwanawe mdogo. Akamvika pia ngozi za wale wanambuzi mikononi na kwenye sehemu laini shingoni mwake. Kisha akampa kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ametayarisha. Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?” Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.” Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”
Mwanzo 27:14-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate aliouandaa. Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Inuka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha.
Mwanzo 27:14-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate alioufanya. Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha.
Mwanzo 27:14-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo alienda akawaleta, akampa mama yake, naye Rebeka akaandaa chakula kitamu, kile alichokipenda baba yake. Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka. Yakobo akaenda kwa baba yake, akasema, “Baba yangu.” Akajibu, “Naam, mwanangu. Wewe ni nani?” Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili unibariki.” Isaka akamuuliza mwanawe, “Umepataje mawindo haraka hivi, mwanangu?” Akajibu, “BWANA Mungu wako amenifanikisha.”