Mhubiri 9:13-18
Mhubiri 9:13-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Pia hapa duniani nimeona mfano wa hekima, na ulionekana kwangu kuwa wenye maana sana. Palikuwa na mji mmoja mdogo wenye wakazi wachache. Mfalme mmoja mwenye nguvu akafika, akauzingira na kujiandaa kuushambulia. Katika mji huo, alikuwapo maskini mmoja mwenye hekima, ambaye, kwa hekima yake aliuokoa mji huo. Lakini hakuna mtu aliyemkumbuka huyo maskini baadaye. Basi, mimi nasema, hekima ni bora kuliko nguvu, ingawa hekima ya maskini haithaminiwi, na maneno yake hayasikilizwi. Afadhali kusikiliza maneno matulivu ya mwenye hekima, kuliko kusikiliza kelele za mfalme katika kikao cha wapumbavu. Kuwa na hekima ni bora kuliko kutegemea silaha, lakini mwenye dhambi mmoja huharibu mazuri mengi.
Mhubiri 9:13-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Pia nimeona mfano huu wa hekima chini ya jua, nao ni kama hivi, tena kwangu mimi ulionekana kuwa neno kubwa. Palikuwa na mji mdogo, uliokuwa na watu wachache ndani yake; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga. Basi, kulikuwemo na mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu yeyote aliyemkumbuka yule mtu maskini. Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; lakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi. Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa, Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu. Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita; Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.
Mhubiri 9:13-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Pia nimeona hekima chini ya jua, nayo ni kama hivi, tena kwangu mimi ilionekana kuwa ni neno kubwa. Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga. Basi, kulionekana humo mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu ye yote aliyemkumbuka yule mtu maskini. Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi. Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa, Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu. Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita; Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.
Mhubiri 9:13-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Pia niliona chini ya jua mfano huu wa hekima ambao ulinivutia sana: Palikuwa na mji mdogo uliokuwa na watu wachache ndani yake. Mfalme mwenye nguvu akainuka dhidi yake, akauzingira kwa jeshi kubwa. Katika mji huo kulikuwa na mtu mmoja maskini lakini mwenye hekima, naye akauokoa ule mji kwa hekima yake. Lakini hakuna aliyemkumbuka yule maskini. Kwa hiyo, nikasema, “Hekima ni bora kuliko nguvu.” Lakini hekima ya maskini imedharauliwa, wala hakuna anayesikiliza maneno yake. Maneno ya utulivu ya mwenye hekima husikiwa kuliko makelele ya mtawala wa wapumbavu. Hekima ni bora kuliko silaha za vita, lakini mwenye dhambi mmoja huharibu mema mengi.