Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 15:1-11

Kumbukumbu la Sheria 15:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

“Kila mwisho wa mwaka wa saba mtawasamehe wadeni wenu wote. Hivi ndivyo mtakavyofanya: Kila mmoja aliyemkopesha jirani yake, alifute hilo deni, wala asijaribu kumdai kwa sababu Mwenyezi-Mungu mwenyewe ameamua deni hilo lifutwe. Mnaweza kuwadai wageni, lakini madeni yote ya ndugu zenu wenyewe mtayafuta. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika nchi anayowapa iwe mali yenu. Hakuna hata mmoja atakayekuwa maskini kati yenu, mradi tu mumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kufuata kwa uangalifu amri ninazowapeni hivi leo. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawabariki kama vile alivyowaahidi. Nanyi mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. Kadhalika mtatawala mataifa mengi, lakini mataifa hayo hayatawatawala nyinyi. “Kukiwa na maskini wa jamaa yenu katika miji ya nchi ambayo Mwenyezi-Mungu atawapa, msiwe wachoyo na wagumu kwake. Badala yake, fumbueni mikono yenu na kumkopesha kwa hiari kiasi cha kutosha mahitaji yake. Angalieni wazo ovu lisiwaingie mioyoni mwenu, mkasema: ‘Mwaka wa saba, mwaka wa kusamehe wadeni, uko karibu’; mkamfikiria ndugu yenu maskini kwa ukali na kukataa kumpa chochote; yeye aweza kumlilia Mwenyezi-Mungu dhidi yenu na hiyo ikawa dhambi kwenu. Mpeni ndugu maskini kwa ukarimu bila kunungunika; maana kwa ajili ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika kazi zenu zote na katika kila mfanyalo. Maana maskini hawatakosekana nchini; hivyo nawaamuru, muwe wakarimu kwa ndugu zenu wahitaji na maskini nchini mwenu.

Kumbukumbu la Sheria 15:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio. Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya BWANA. Waweza kumtoza mgeni; lakini kila uwiacho kwa nduguyo mkono wako utamwachilia. Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa BWANA atakubarikia kweli katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;) kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya. Kwani BWANA, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao. Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini; lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo. Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; jicho lako likawa ovu juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia BWANA juu yako, ikawa ni dhambi kwako. Mpe kwa kweli, wala moyo wako usisikitike utakapompa; kwa kuwa atakubarikia BWANA, Mungu wako, kwa neno hili katika kazi yako yote, na katika kila utakalotia mkono wako. Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.

Kumbukumbu la Sheria 15:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kumbukumbu la Sheria 15:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa BWANA wa kufuta madeni umetangazwa. Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. Hata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi BWANA Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, ikiwa tutamtii BWANA Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. Kwa kuwa BWANA Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi. Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo BWANA Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia BWANA dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili BWANA Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. Siku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha