Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Torati 15:1-11

Kumbukumbu la Torati 15:1-11 SRUV

Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio. Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya BWANA. Waweza kumtoza mgeni; lakini kila uwiacho kwa nduguyo mkono wako utamwachilia. Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa BWANA atakubarikia kweli katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;) kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya. Kwani BWANA, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao. Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini; lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo. Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; jicho lako likawa ovu juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia BWANA juu yako, ikawa ni dhambi kwako. Mpe kwa kweli, wala moyo wako usisikitike utakapompa; kwa kuwa atakubarikia BWANA, Mungu wako, kwa neno hili katika kazi yako yote, na katika kila utakalotia mkono wako. Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha