Danieli 4:1-18
Danieli 4:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mimi mfalme Nebukadneza, nawaandikia watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote kote duniani. Nawatakieni amani tele! Nimeona vema kuwajulisha ishara na maajabu ambayo Mungu Mkuu amenionesha. Jinsi gani zilivyo kubwa ishara zake Mungu! Maajabu yake ni makuu mno! Ufalme wake ni ufalme wa milele; enzi yake yadumu kizazi hata kizazi. “Mimi, Nebukadneza, nilikuwa ninaishi raha mstarehe nyumbani kwangu na kufana katika ikulu yangu. Lakini nikaota ndoto iliyonitisha; nikiwa nimelala kitandani, mawazo na maono kichwani mwangu yaliniogopesha. Hivyo, nikaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waletwe mbele yangu ili wanieleze maana ya ndoto hiyo. Ndipo waganga, walozi, Wakaldayo na wanajimu wakaletwa. Nikawasimulia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunieleza maana yake. Baadaye, akaja Danieli, anayeitwa pia Belteshaza, jina la mungu wangu, ambaye roho ya miungu mitakatifu imo ndani yake. Nami nikamsimulia ndoto yangu, nikasema: Ee Belteshaza, uliye mkuu wa waganga, nafahamu kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako, na kwamba hakuna fumbo lililo gumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu; niambie maana yake. “Nilipokuwa nimelala, niliona maono haya: Niliona mti mrefu sana katikati ya dunia. Mti uliendelea kukua, ukawa imara na kilele chake kikafika mbinguni. Uliweza kuonekana kutoka kila mahali duniani. Majani yake yalikuwa mazuri. Ulikuwa umejaa matunda, kiasi cha kuitosheleza dunia nzima. Wanyama wote wa porini walipata kivuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake. Viumbe vyote vilipata chakula kutoka mti huo. “Nilipokuwa nimelala kitandani, niliona maono: Mlinzi mtakatifu alishuka kutoka mbinguni. Akapaaza sauti akisema, ‘Kateni mti huu na kuyakatakata matawi yake. Pukuteni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na watoroke chini yake na ndege kutoka matawi yake. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini, kwenye majani mabichi ya kondeni kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini na kula nyasi mbugani. Akili yake ya utu ibadilishwe, awe na akili ya mnyama kwa miaka saba. Hii ni hukumu iliyotangazwa na walinzi; ni uamuzi wa walio watakatifu, ili wanaadamu wote kila mahali wapate kutambua kuwa Mungu Mkuu anayo mamlaka juu ya falme zote za wanaadamu; yeye humpa ufalme mtu yeyote ampendaye, humfanya mfalme hata mtu duni wa mwisho.’ “Hii ndiyo ndoto niliyoota mimi Nebukadneza. Sasa, wewe Belteshaza, nieleze maana yake; kwani wenye hekima wote katika ufalme wangu hawawezi kuniambia maana yake; lakini wewe utaweza kwa kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako.”
Danieli 4:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme Nebukadneza, kwa watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wanaokaa katika dunia yote; Amani iongezeke kwenu. Mimi nimeona vema kutangaza habari za ishara na maajabu, aliyonitendea Mungu aliye juu. Ishara zake ni kubwa kama nini! Na maajabu yake yana uweza kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi. Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nikistarehe nyumbani kwangu, nikineemeka katika nyumba yangu ya enzi. Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha. Basi nikatoa amri kwamba wenye hekima wote wa Babeli, waletwe mbele yangu, ili kunijulisha tafsiri ya ndoto ile. Ndipo wakaingia waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; nikawahadithia ile ndoto; wao wasiweze kunijulisha tafsiri yake. Bali hatimaye Danieli akaingia mbele yangu, ambaye jina lake ni Belteshaza, kwa kufuata jina la mungu wangu; tena ndani yake inakaa roho ya miungu watakatifu; nikamsimulia ile ndoto, nikisema, Ee Belteshaza, mkuu wa waaguzi, kwa sababu ninajua ya kuwa roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako, na ya kuwa hapana neno la siri likushindalo, niambie maana ya hii ndoto yangu niliyoiona, na tafsiri yake. Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi; niliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana. Mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia. Majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote; wanyama wa mwituni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake; kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake. Nikaona katika njozi za kichwa changu kitandani mwangu, na tazama, mlinzi, naye ni mtakatifu, alishuka kutoka mbinguni. Akapaza sauti yake, akasema, Ukateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yapukusieni mbali majani yake, na kuyatawanya matunda yake, wanyama na waondoke hapo chini yake, na ndege katika matawi yake. Lakini kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikapate maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama katika majani ya nchi; moyo wake ubadilike, usiwe moyo wa binadamu, na apewe moyo wa mnyama; nyakati saba zikapite juu yake. Hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye Juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge. Mimi, Nebukadneza, nimeiona ndoto hii; na wewe, Ee Belteshaza, eleza tafsiri yake, kwa maana wenye hekima wote wa ufalme wangu hawawezi kunijulisha tafsiri yake; bali wewe waweza, maana roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako.
Danieli 4:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mfalme Nebukadreza, kwa watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wanaokaa katika dunia yote; Amani iongezeke kwenu. Mimi nimeona vema kutangaza habari za ishara na maajabu, aliyonitendea Mungu aliye juu. Ishara zake ni kubwa kama nini! Na maajabu yake yana uweza kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi. Mimi, Nebukadreza, nalikuwa nikistarehe katika nyumba yangu, nikisitawi katika nyumba yangu ya enzi. Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha. Basi nikatoa amri kwamba wenye hekima wote wa Babeli, waletwe mbele yangu, ili kunijulisha tafsiri ya ndoto ile. Ndipo wakaingia waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; nikawahadithia ile ndoto; wao wasiweze kunijulisha tafsiri yake. Bali hatimaye Danieli akaingia mbele yangu, ambaye jina lake ni Belteshaza, kwa kufuata jina la mungu wangu; tena ndani yake inakaa roho ya miungu watakatifu; nikamhadithia ile ndoto, nikisema, Ee Belteshaza, mkuu wa waganga, kwa sababu ninajua ya kuwa roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako, na ya kuwa hapana neno la siri likushindalo, niambie njozi za ndoto yangu niliyoiona, na tafsiri yake. Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi; naliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana. Mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia. Majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote; wanyama wa kondeni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake; kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake. Nikaona katika njozi za kichwa changu kitandani mwangu, na tazama, mlinzi, naye ni mtakatifu, alishuka kutoka mbinguni. Akapaza sauti yake, akasema, Ukateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yapukusieni mbali majani yake, na kuyatawanya matunda yake, wanyama na waondoke hapo chini yake, na ndege katika matawi yake. Walakini kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikapate maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama katika majani ya nchi; moyo wake ubadilike, usiwe moyo wa binadamu, na apewe moyo wa mnyama; nyakati saba zikapite juu yake. Hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge. Mimi, Nebukadreza, nimeiona ndoto hii; na wewe, Ee Belteshaza, eleza tafsiri yake, kwa maana wenye hekima wote wa ufalme wangu hawawezi kunijulisha tafsiri yake; bali wewe waweza, maana roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako.
Danieli 4:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mfalme Nebukadneza, Kwa watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wanaoishi duniani kote: Mafanikio yawe kwenu sana! Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara za miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia. Ishara zake ni kuu kama nini! Na maajabu yake yana nguvu kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; enzi yake hudumu kizazi hadi kizazi. Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nyumbani katika jumba langu la kifalme, nikiishi kwa raha na mafanikio. Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita mawazoni mwangu vilinitisha. Hivyo nikaagiza kwamba wenye hekima wote wa Babeli waletwe mbele yangu kunifasiria ndoto yangu. Waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi walipokuja, niliwaambia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunifasiria. Mwishoni, Danieli alikuja mbele yangu, nikamweleza hiyo ndoto. (Danieli anaitwa Belteshaza, kwa jina la mungu wangu, nayo roho ya miungu mitakatifu inakaa ndani yake.) Nikasema, “Belteshaza, mkuu wa waganga, ninajua kuwa roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako, wala hakuna siri iliyo ngumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu, nifasirie. Haya ndio maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana. Mti ule ulikua, ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga; ulionekana hadi miisho ya dunia. Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi, na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo. “Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, na mbele yangu nikaona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni. Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, myafyeke matawi yake; yaondoeni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake, na ndege waondoke kutoka matawi yake. Lakini kiacheni kisiki na mizizi yake, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni. “ ‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia. Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu, na apewe akili ya mnyama, hadi nyakati saba zipite juu yake. “ ‘Uamuzi huu umetangazwa na wajumbe; watakatifu, wametangaza hukumu ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za dunia, naye humpa amtakaye, na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’ “Hii ndiyo ndoto niliyoipata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe unaweza, kwa sababu roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako.”