Danieli 4:1-18
Danieli 4:1-18 NENO
Mfalme Nebukadneza, Kwa watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wanaoishi duniani kote: Mafanikio yawe kwenu sana! Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara za miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia. Ishara zake ni kuu kama nini! Na maajabu yake yana nguvu kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; enzi yake hudumu kizazi hadi kizazi. Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nyumbani katika jumba langu la kifalme, nikiishi kwa raha na mafanikio. Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita mawazoni mwangu vilinitisha. Hivyo nikaagiza kwamba wenye hekima wote wa Babeli waletwe mbele yangu kunifasiria ndoto yangu. Waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi walipokuja, niliwaambia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunifasiria. Mwishoni, Danieli alikuja mbele yangu, nikamweleza hiyo ndoto. (Danieli anaitwa Belteshaza, kwa jina la mungu wangu, nayo roho ya miungu mitakatifu inakaa ndani yake.) Nikasema, “Belteshaza, mkuu wa waganga, ninajua kuwa roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako, wala hakuna siri iliyo ngumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu, nifasirie. Haya ndio maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana. Mti ule ulikua, ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga; ulionekana hadi miisho ya dunia. Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi, na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo. “Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, na mbele yangu nikaona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni. Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, myafyeke matawi yake; yaondoeni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake, na ndege waondoke kutoka matawi yake. Lakini kiacheni kisiki na mizizi yake, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni. “ ‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia. Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu, na apewe akili ya mnyama, hadi nyakati saba zipite juu yake. “ ‘Uamuzi huu umetangazwa na wajumbe; watakatifu, wametangaza hukumu ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za dunia, naye humpa amtakaye, na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’ “Hii ndiyo ndoto niliyoipata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe unaweza, kwa sababu roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako.”