Wakolosai 1:3-14
Wakolosai 1:3-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho. Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi
Wakolosai 1:3-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. Maana tumesikia juu ya imani yenu kwa Kristo Yesu na juu ya mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu. Imani yenu na mapendo yenu vina msingi katika tumaini mlilowekewa mbinguni. Mlipata kusikia juu ya hilo tumaini mara ya kwanza wakati mlipohubiriwa ule ujumbe wa ukweli wa Habari Njema. Injili inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu nyinyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli. Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho. Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu wakati tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa matakwa yake, pamoja na hekima yote na ujuzi wa kiroho. Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu. Na kwa furaha mshukuruni Baba, aliyewawezesha nyinyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale aliyowawekea watu wake katika ufalme wa mwanga. Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi. Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Wakolosai 1:3-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mwenzi wetu mpendwa, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho. Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na subira ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa kutoka kwa nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.
Wakolosai 1:3-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunapowaombea ninyi, kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote: imani na upendo ule utokao katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni, na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani, ile Injili iliyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote. Mlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, yeye aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu, ambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho. Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.