Wakolosai 1:21-29
Wakolosai 1:21-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo kwanza nyinyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa maadui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu. Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awaweke mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama. Mnapaswa, lakini kuendelea na msingi imara katika imani, wala msikubali kutikiswa kutoka katika tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Injili ambayo imekwisha hubiriwa kila mtu duniani. Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa. Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake, ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake. Mungu ametaka kuwajulisha hao jinsi siri hiyo ilivyo kuu na tukufu ambayo imeenea kwa watu wa mataifa, nayo ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba nyinyi mtaushiriki utukufu wa Mungu. Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo. Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.
Wakolosai 1:21-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmetengwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa kwa viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nilikuwa mhudumu wake. Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake; ambalo nimefanywa mhudumu wake, kulingana na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo. Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu.
Wakolosai 1:21-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa mhudumu wake. Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake; ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo. Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu.
Wakolosai 1:21-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kupitia kwa mwili wa Kristo kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama, ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake. Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa. Mimi nimekuwa mtumishi wa kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi neno la Mungu kwa ukamilifu: Hii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. Kwao Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu. Yeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo. Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.