Wakolosai 1:1-23
Wakolosai 1:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu. Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. Maana tumesikia juu ya imani yenu kwa Kristo Yesu na juu ya mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu. Imani yenu na mapendo yenu vina msingi katika tumaini mlilowekewa mbinguni. Mlipata kusikia juu ya hilo tumaini mara ya kwanza wakati mlipohubiriwa ule ujumbe wa ukweli wa Habari Njema. Injili inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu nyinyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli. Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho. Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu wakati tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa matakwa yake, pamoja na hekima yote na ujuzi wa kiroho. Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu. Na kwa furaha mshukuruni Baba, aliyewawezesha nyinyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale aliyowawekea watu wake katika ufalme wa mwanga. Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi. Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Maana kwake vitu vyote viliumbwa kila kitu duniani na mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: Wenye enzi, watawala, wakuu na wenye nguvu. Vyote viliumbwa kwake na kwa ajili yake. Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote; vyote huendelea kuwako kwa uwezo wake. Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote. Maana Mungu alipenda utimilifu wake wote uwe ndani yake. Kwake vitu vyote vilipatanishwa na Mungu: Na kwa damu yake msalabani akafanya amani na vitu vyote duniani na mbinguni. Hapo kwanza nyinyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa maadui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu. Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awaweke mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama. Mnapaswa, lakini kuendelea na msingi imara katika imani, wala msikubali kutikiswa kutoka katika tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Injili ambayo imekwisha hubiriwa kila mtu duniani.
Wakolosai 1:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo, ndugu yetu, kwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Kristo, walioko Kolosai. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu. Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mwenzi wetu mpendwa, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho. Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na subira ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa kutoka kwa nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi. Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au milki, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni. Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmetengwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa kwa viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nilikuwa mhudumu wake.
Wakolosai 1:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo, ndugu yetu, kwa ndugu watakatifu, waaminifu katika Kristo, walioko Kolosai. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu. Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho. Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni. Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa mhudumu wake.
Wakolosai 1:1-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu. Kwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Kristo wanaoishi Kolosai. Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba yetu ziwe nanyi. Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunapowaombea ninyi, kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote: imani na upendo ule unaotoka katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni, na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani ile Injili iliyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote. Mlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu, ambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho. Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake Mpendwa, ambaye kwake tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi. Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwake yeye vitu vyote vilivyo mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya utawala au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa kupitia kwake na kwa ajili yake. Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, na kupitia kwake aweze kuvipatanisha vitu vyote kwake mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake iliyomwagika msalabani. Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kupitia kwa mwili wa Kristo kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama, ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake.