Amosi 5:1-27
Amosi 5:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni maombolezo yangu juu yenu, enyi Waisraeli: Umeanguka na hutainuka tena ewe binti Israeli! Umeachwa pweke nchini mwako, hamna hata mtu wa kukuinua. Maana Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu 1,000 watatoka mjini kwenda kupigana lakini watarejea 100 tu; wataondoka watu 100 wa kijiji kimoja lakini watanusurika watu kumi tu.” Mwenyezi-Mungu awaambia hivi Waisraeli: “Nitafuteni mimi nanyi mtaishi! Lakini msinitafute huko Betheli wala msiende Gilgali wala msivuke kwenda Beer-sheba. Maana wakazi wa Gilgali, hakika watachukuliwa uhamishoni, na Betheli utaangamizwa!” Mtafuteni Mwenyezi-Mungu, nanyi mtaishi! La sivyo, atawalipukia wazawa wa Yosefu kama moto; moto utawateketeza wakazi wa Betheli na hakuna mtu atakayeweza kuuzima. Tahadhari enyi mnaogeuza haki kuwa uchungu, na kuuona uadilifu kuwa kama takataka! Huyo aliyezifanya Kilimia na sayari Orioni, ambaye huligeuza giza nene kuwa mchana, na mchana kuwa usiku; yeye ambaye ayaitaye pamoja maji ya bahari na kuyamwaga juu ya nchi kavu, Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake. Yeye ndiye anayewaangamiza wenye nguvu, na kuziharibu ngome zao. Nyinyi huwachukia watetezi wa haki na wenye kusema ukweli mahakamani. Nyinyi mnawakandamiza fukara na kuwatoza kodi ya ngano kupita kiasi. Mnajijengea nyumba za mawe ya kuchonga, lakini nyinyi hamtaishi humo; mnalima bustani nzuri za mizabibu, lakini hamtakunywa divai yake. Maana mimi najua wingi wa makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu; nyinyi mnawatesa watu wema, mnapokea rushwa na kuzuia fukara wasipate haki mahakamani. Basi, kutakuwa na wakati mbaya ambao hata mwenye busara atanyamaza. Tafuteni kutenda mema na si mabaya, ili nyinyi mpate kuishi naye Mwenyezi-Mungu wa majeshi awe pamoja nanyi kama mnavyosema. Chukieni uovu, pendeni wema, na kudumisha haki mahakamani. Yamkini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawafadhili watu wa Yosefu waliobaki. Basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, naam, Mwenyezi-Mungu asema: “Patakuwa na kilio kila mahali mitaani; watu wataomboleza: ‘Ole! Ole!’ Wakulima wataitwa waje kuomboleza, na mabingwa wa kuomboleza waje kufanya matanga. Patakuwa na kilio katika mashamba yote ya mizabibu; maana nitapita kati yenu kuwaadhibu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.” Ole wenu nyinyi mnaoingojea kwa hamu siku ya Mwenyezi-Mungu! Kwa nini mnaitaka sana siku hiyo? Siku hiyo, itakuwa siku ya giza na sio ya mwanga! Mambo yatakuwa kama mtu aliyekimbia simba, halafu akakumbana na dubu! Au kama mtu anayerudi nyumbani kwake, akatia mkono ukutani, akaumwa na nyoka. Siku ya Mwenyezi-Mungu itakuwa giza, na sio mwanga; itakuwa huzuni bila uangavu wowote. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nazichukia na kuzidharau sikukuu zenu; siifurahii mikutano yenu ya kidini. Mjaponitolea sadaka zenu za kuteketezwa na za nafaka, mimi sitakubali kuzipokea; na sadaka zenu za amani za wanyama wanono mimi sitaziangalia kabisa. Ondoeni mbele yangu kelele za nyimbo zenu! Sitaki kusikiliza muziki wa vinubi vyenu! Lakini acheni haki itiririke kama maji, uadilifu uwe kama mto usiokauka. “Enyi Waisraeli, wakati ule mlipokuwa kule jangwani kwa miaka arubaini, je, mliniletea tambiko na sadaka hata mara moja? Je, wakati huo mlibeba kama sasa vinyago vya mungu wenu Sakuthi mfalme wenu na vinyago vya Kaiwani mungu wenu wa nyota, vitu ambavyo mlijitengenezea wenyewe? Kwa hiyo nitawapeleka uhamishoni, mbali kuliko Damasko! Hayo amesema Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mungu wa Majeshi.
Amosi 5:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lisikieni neno hili nilitamkalo liwe maombolezo juu yenu, enyi nyumba ya Israeli. Bikira wa Israeli ameanguka; hatainuka tena; Ameangushwa katika nchi yake; hakuna mtu wa kumwinua. Kwa kuwa Bwana MUNGU asema hivi; Mji uliotoka nje wenye watu elfu moja, utabakiziwa watu mia moja, na mji uliotoka wenye watu mia moja, utabakiziwa watu kumi, kwa nyumba ya Israeli. Maana BWANA awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi; bali msitafute Betheli, wala msiingie Gilgali, wala msipite kwenda Beer-sheba; kwani Gilgali hakika yake itakwenda utumwani, na Betheli itakuwa ubatili. Mtafuteni BWANA, nanyi mtaishi; asije akawaka kama moto katika nyumba ya Yusufu, nao ukateketeza, asiwepo mtu awezaye kuuzima katika Betheli. Ninyi mnaogeuza hukumu kuwa uchungu, na kuiangusha haki chini, mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA, ndilo jina lake; yeye aletaye uharibifu wa ghafla juu ya wenye nguvu, hata kuiharibu ngome. Wao humchukia yeye akemeaye langoni, nao humzira anenaye maneno ya adili. Basi, kwa kuwa mnamkanyaga maskini, na kumtoza ngano; ninyi mmejenga nyumba za mawe yaliyochongwa, lakini hamtakaa ndani yake; ninyi mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, lakini hamtakunywa divai yake. Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao. Kwa ajili ya hayo mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo; kwa kuwa ni wakati mbaya. Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo BWANA, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo. Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba BWANA, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu. Kwa ajili ya hayo, asema BWANA, Mungu wa majeshi, aliye Bwana; Kutakuwako maombolezo katika njia kuu zote; nao watasema katika njia zote, Ole! Ole! Nao watamwita mkulima aje kuombolea, na hao walio hodari wa kulia waje kuomboleza. Tena katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwako kulia; kwa maana mimi nitapita katikati yako, asema BWANA. Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwa nini kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru. Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga. Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu. Lakini hukumu na iteremke kama maji, na haki kama maji makuu. Je! Mliniletea dhabihu na sadaka jangwani muda wa miaka arubaini, enyi nyumba ya Israeli? Naam, mtamchukua Sikuthi, mfalme wenu, na Kiuni, sanamu zenu, nyota ya mungu wenu, mliojifanyia wenyewe. Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni, mwende mbali kupita Dameski, asema BWANA, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.
Amosi 5:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lisikieni neno hili nilitamkalo liwe maombolezo juu yenu, enyi nyumba ya Israeli. Bikira wa Israeli ameanguka; hatainuka tena; Ameangushwa katika nchi yake; hakuna mtu wa kumwinua. Kwa kuwa Bwana MUNGU asema hivi; Mji uliotoka nje wenye watu elfu, utasaziwa watu mia, na mji uliotoka wenye watu mia, utasaziwa watu kumi, kwa nyumba ya Israeli. Maana BWANA awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi; bali msitafute Betheli, wala msiingie Gilgali, wala msipite kwenda Beer-sheba; kwani Gilgali hakika yake itakwenda utumwani, na Betheli itakuwa ubatili. Mtafuteni BWANA, nanyi mtaishi; asije akawaka kama moto katika nyumba ya Yusufu, nao ukateketeza, asiwepo mtu awezaye kuuzima katika Betheli. Ninyi mnaogeuza hukumu kuwa uchungu, na kuiangusha haki chini, mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA, ndilo jina lake; yeye aletaye uharibifu wa ghafula juu yao walio hodari, hata uharibifu uipate ngome. Wao humchukia yeye akemeaye langoni, nao humzira anenaye maneno ya adili. Basi, kwa kuwa mnamkanyaga maskini, na kumtoza ngano; ninyi mmejenga nyumba za mawe yaliyochongwa, lakini hamtakaa ndani yake; ninyi mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, lakini hamtakunywa divai yake. Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao. Kwa ajili ya hayo mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo; kwa kuwa ni wakati mbaya. Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo BWANA, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo. Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba BWANA, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu. Kwa ajili ya hayo, asema BWANA, Mungu wa majeshi, aliye Bwana; Kutakuwako maombolezo katika njia kuu zote; nao watasema katika njia zote, Ole! Ole! Nao watamwita mkulima aje kuombolea, na hao walio hodari wa kulia waje kuomboleza. Tena katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwako kulia; kwa maana mimi nitapita katikati yako, asema BWANA. Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwani kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru. Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga. Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu. Lakini hukumu na itelemke kama maji, na haki kama maji makuu. Je! Mliniletea dhabihu na sadaka jangwani muda wa miaka arobaini, enyi nyumba ya Israeli? Naam, mtamchukua Sikuthi, mfalme wenu, na Kiuni, sanamu zenu, nyota ya mungu wenu, mliojifanyizia wenyewe. Kwa sababu hiyo nitawahamisha, hali ya kufungwa, mwende mbali kupita Dameski, asema BWANA, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.
Amosi 5:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi: “Bikira Israeli ameanguka, kamwe hatainuka tena, ameachwa pweke katika nchi yake, hakuna yeyote wa kumwinua.” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “Mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli, mia moja tu watarudi; wakati mji utakapopeleka mia moja, kumi tu ndio watarudi hai.” Hili ndilo asemalo BWANA kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni mpate kuishi; msitafute Betheli, msiende Gilgali, msisafiri kwenda Beer-Sheba. Kwa maana kwa hakika Gilgali itaenda uhamishoni, na Betheli itafanywa kuwa ubatili.” Mtafuteni BWANA mpate kuishi, au atafagia nyumba ya Yusufu kama moto; utawateketeza, nayo Betheli haitakuwa na yeyote wa kuuzima. Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu na kuiangusha haki chini (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni, ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko na mchana kuwa usiku, ambaye huyaita maji ya bahari na kuyamwaga juu ya nchi: BWANA ndilo jina lake; yeye hufanya maangamizi kwenye ngome na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa), mnamchukia yule akemeaye mahakamani, na kumdharau yule ambaye husema kweli. Mnamgandamiza maskini na kumlazimisha awape nafaka. Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari, hamtaishi ndani yake; ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, hamtakunywa divai yake. Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu. Mmewadhulumu wenye haki na kupokea rushwa na kuzuia haki ya maskini mahakamani. Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza nyakati kama hizo, kwa kuwa nyakati ni mbaya. Tafuteni mema, wala si mabaya, ili mpate kuishi. Ndipo BWANA Mungu wa majeshi atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo yupo nanyi. Yachukieni maovu, yapendeni mema; dumisheni haki mahakamani. Yamkini BWANA Mungu wa majeshi atawahurumia mabaki ya Yusufu. Kwa hiyo hili ndilo Bwana, BWANA Mungu wa majeshi, asemalo: “Kutakuwa na maombolezo barabarani zote, na vilio vya uchungu katika njia kuu zote. Wakulima wataitwa kuja kulia, na waombolezaji waje kuomboleza. Kutakuwa na kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu, kwa kuwa nitapita kati yenu,” asema BWANA. BWANA Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya BWANA! Kwa nini mnaitamani siku ya BWANA? Siku hiyo itakuwa giza, si nuru. Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba kumbe akakutana na dubu, kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta, kumbe akaumwa na nyoka. Je, siku ya BWANA haitakuwa giza, na si nuru: giza nene, bila mwali wowote? “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini; siwezi kuvumilia makusanyiko yenu. Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka, sitazikubali. Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani, sitazitambua. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu! Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu. Lakini acheni haki itiririke kama mto, na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka! “Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli? Mmeyainua madhabahu ya Sikuthi mungu wenu mtawala, na Kiuni mungu wenu wa nyota, ambao mliwatengeneza wenyewe. Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,” asema BWANA, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.